Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na
Kimataifa, Dk Augustine Mahiga amemtetea Rais John Magufuli kwa
kutohudhuria hafla ya mwaka ya mabalozi akisema alikuwa Singida kwenye
maadhimisho ya miaka 39 ya CCM.
Balozi Mahiga alikuwa mgeni
rasmi kwenye hafla hiyo iliyofanyika Ikulu ya kukaribisha mwaka mpya wa
mabalozi ambayo kwa kawaida mwenyeji huwa ni Rais.
Dk Mahiga
alitoa ufafanuzi huo kwa waandishi wa habari jana baada ya kuulizwa
sababu za Rais kushindwa kuhudhuria hafla hiyo, lakini maelezo hayo
yalichanganya zaidi, kwa kuwa hafla hiyo ya mabalozi ilifanyika Februari
8 wakati kilele cha sherehe za CCM kilikuwa Februari 6.
Kuhusu
tofauti hiyo ya siku, Dk Mahiga alisema baada ya sherehe ya Singida,
Rais alipitia kwenye ziara ambayo hata hivyo hakuifafanua.
Wakati
huohuo, Waziri Mahiga alisema licha ya Dk Magufuli kuwakilishwa kwenye
mikutano katika nchi mbalimbali, nchi hizo zinafahamu anachokifanya na
bado nchi inaheshimika.
Akitoa mfano, katika mkutano wa wakuu wa
nchi za Afrika ulioandaliwa na China ambao ulifanyika Afrika Kusini,
alisema licha ya Tanzania kuwakilishwa na makamu wa Rais, Samia Suluhu
Hassan, ilikuwa miongoni mwa nchi nne kati ya 54 za Afrika zilizopewa
kipaumbele na kuwekeza katika sekta ya viwanda. Nchi nyingine zilizopewa
kipaumbele ni Kenya, Ethiopia na Afrika Kusini.
“Utaona namna
tunavyokubalika kimataifa kati ya nchi 54 za Afrika tunakuwa miongoni wa
nchi nne zitakazopewa kipaumbele,” alisema.
Alisema wizara yake itaendelea kubana matumizi kwa kuziwezesha balozi za nje ili ziwe na uwakilishi imara.
Akitoa
mfano, Dk Mahiga alisema juzi alirejea kutoka Angola ambako
alimwakilisha Rais Magufuli kwenye mkutano wa Maziwa Makuu, akiongozana
na watu watatu tofauti na zamani ambako angekuwa na msururu wa watu.
Alisema
hata Makamu wa Rais alipokwenda Ethiopia kwenye mkutano wa Umoja wa
Afrika (AU) alisafiri na watu 14 wakati zamani angesafiri na zaidi ya
watu 30.
Post a Comment