Viongozi wa Kiislamu nchini Uganda
wamepinga wazo la mgombea urais Amama Mbabazi la kutaka kurejesha mwili
wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Idi Amin .
Viongozi hao wamesema hatua ya Bw Amin kuzikwa Mecca ni hadhi kubwa katika Uislamu.Aidha wamesema dini ya Kiislamu haikubali mwili wa mtu kufukuliwa na kuzikwa tena.
Msemaji wa Baraza Kuu la Waislamu Uganda Hajj Nsereko Mutumba ameambia BBC kwamba haamini Bw Mbabazi alikuwa na nia ya dhati alitoa ahadi hiyo.
“Kusema eti atarejesha maiti yake, huo ni uongo. Cha kwanza alikuwa waziri wa ulinzi kwa miaka mingi. Pili, alikuwa ndiye kiongozi wa sera wa NRM (chama tawala cha National Resistance Movement), alikuwa mtu mkubwa kwa NRM,” amesema.
Bw Mutumba amesema tangazo la Bw Mbabazi “ni siasa tu” kwa sababu hajatangamana na jamii ya Waislamu sana.
Bw Mbabazi, aliyekuwa waziri mkuu kati ya 2011-2014, ni miongoni mwa wagombea saba wanaojaribu kufikisha kikomo uongozi wa miaka 30 wa Rais Yoweri Museveni.
Alitoa ahadi yake alipotembelea eneo alikozaliwa marehemu Amin kaskazini magharibi mwa Uganda ambapo alilakiwa na mjombake kiongozi huyo wa zamani.
Abed Bwanika, aliyewania urais na kushindwa mara tatu, alitoa ahadi sawa alipozuru eneo hilo.
Idi Amin aliondolewa madarakani 1979. Alitorokea Libya kwanza kisha akaelekea Saudi Arabia ambako aliishi uhamisho hadi kifo chake tarehe 16 Agosti, 2003.
Post a Comment