Monday, 22 February 2016
TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI LILILOTOLEWA NA MHE. DR. HAMISI A. KIGWANGALLA (MB); NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, TAREHE 22 FEBRUARI 2016
Posted by Unknown on 21:38:00 in | Comments : 0
Ndugu Waandishi wa Habari,
Taarifa hii ni mwendelezo wa utaratibu ambao Wizara imejiwekea kila wiki wa kutoa taarifa kwa umma kuhusu hali ya kipindupindu nchini ikiwa ni pamoja na kueleza juhudi mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa ili kukabiliana na hali hii. Hadi kufikia tarehe 21 Februari 2016, jumla ya watu 16,352 wameugua ugonjwa huo, na kati yao watu 249 wamepoteza maisha.
Takwimu za wiki iliyopita zinaonyesha kuwa kuanzia tarehe 15 hadi 21 Februari 2016, idadi ya wagonjwa wapya walioripotiwa ni 499 ambapo kati yao watu 6 walipoteza maisha. Idadi ya wagonjwa wiki hii imepungua japo sio kwa kiwango kikubwa (5%) ukilinganisha na wiki iliyoishia tarehe 14 February ambapo wagonjwa 528 waliripotiwa.
Jumla ya mikoa ambayo imeripoti kuwa na wagonjwa kwa wiki iliyopita ni 11, ambapo Mkoa wa Iringa ndio ulioongoza kwa kuripoti idadi kubwa ya wagonjwa yaani wagonjwa 143 (Iringa Vijijini 143) ukifuatiwa na Mwanza 94 (Ilemela 50, Ukerewe 22, Nyamagana 14, Sengerema 1), Mara 87 (Musoma mjini 38, Tarime vijijini 24, Rorya 19, Bunda 4 na Musoma vijijini 2), Dodoma 66 (Chamwino 25, Mpwapwa 23 na Dodoma mjini 18) na Morogoro 42 (Morogoro Manispaa 22, Ulanga 13 na Kilosa 7). Mikoa mingine iliyoripoti wagonjwa ni Mbeya 30, Arusha 17, Dar es Salaam 14, Simiyu 3, Kilimanjaro 2 na Manyara 1.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Wizara bado inaendelea kukumbana na changamoto mbalimbali katika kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu. Vikosi kazi vya wataalamu kutoka wizara yangu wanaoendelea kuzuru maeneo mbalimbali wameendelea kuibua changamoto hizo na kuhakikisha zinafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo ili kuzuia ueneaji wa vimelea vya ugonjwa huu na kisha kuutokomeza kabisa.
Moja ya changamoto kubwa inayoendelea kujitokeza ni pale ambapo baadhi ya wataalamu wa ngazi mbalimbali pamoja na wanajamii wanapowaficha wagonjwa na hivyo kutoa taarifa ya wagonjwa wachache kuliko uhalisia. Madhara yanayoambatana na hili ni kutokuwepo kwa taarifa za kutosha zitakazoongoza juhudi za kuzuia ugonjwa kutoka katika maeneo ambayo wagonjwa hawakutolewa taarifa na hivyo kuongeza hatari ya ugonjwa kuendelea kusambaa kimya kimya na baadae kusababisha wagonjwa wengi kujitokeza katika maeneo hayo kwa mara moja.
Wizara inaendelea kufanya juhudi mbalimbali kuhakikisha kuwa inatokomeza ugonjwa huu wa kipindupindu na inazitaka mamlaka zinazohusika na kuwatambua wagonjwa kushirikiana na kutoa taarifa sahihi kama inavyoelekezwa katika miongozo mbalimbali ya Wizara ikiwamo muongozo wa udhibiti wa magonjwa ya milipuko Tanzania wa mwaka 2011 “IDSR” na muongozo wa udhibiti wa ugonjwa wa kipindupindu toleo la tatu wa mwaka 2015. Pia kwa jamii tunawasihi pale wapatapo wagonjwa wawapeleke katika vituo vyetu vya kutolea huduma ili wapatiwe matibabu sahihi na kutolewa taarifa. Kwa kufanya hivyo taarifa za kutosha na sahihi zitakazosaidia kupambana na kuutokomeza ugonjwa huu zitapatikana kwa wakati na hivyo kuwezesha kuutokomeza ugonjwa huu mapema. Tunatoa rai kwa viongozi hususani ngazi ya Mikoa na Wilaya kutokutoa kauli za kutaka kuwaadhibu watendaji na viongozi wa ngazi za chini kwa kigezo cha wagonjwa kuwepo katika maeneo yao kwani kwa kufanya hivyo wataongeza kasi ya kuficha wagonjwa na hivyo kukwamisha juhudi za kupambana na kipindupindu. Aidha tunatoa wito kwa mikoa yote nchini kuhakikisha kuwa wanaimarisha vikao vya Kamati za Afya ya Msingi (PHC meetings) na kutumia taarifa zinazotokana na uchambuzi wa mwenendo wa ugonjwa katika maeneo yao ili ziwasaidie kupanga mbinu sahihi za udhibiti wa kipindupindu.
Ndugu waandishi wa habari,
Tarehe 15 Februari 2016 nilitembelea kijiji cha Mboliboli kata ya Pawaga Wilaya ya Iringa ambacho kilikumbwa na mafuriko kutoka mto Ruaha yaliyotokana na mvua kubwa kunyesha na maji kuzoa vyoo ambavyo vilitapanya kinyesi katika vijiji vilivyopo kando ya mto uliosababisha mlipuko wa Kipindupindu. Sambamba na hilo Wizara ilituma timu ya wataalamu ili kufanya tathmini na kuongeza nguvu ya kupambana na kuzuia ueneaji wa ugonjwa huu kwa wahanga wa mafuriko. Tunaupongeza Mkoa wa Iringa pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa juhudi wanazoziendeleza za kuutokomezwa ugonjwa huu na kuuzuia usisambae katika maeneo ya jirani. Wizara kwa kushirikiana na wadau mbali mbali itaendelea kutoa msaada wa kitaalamu kwa Mikoa na Halmashauri zote ili kusaidia juhudi zilizopo za kupambana na ugonjwa huu na hatimaye kuutokomeza kabisa.
Tunaendelea kuisihi jamii kuungana na halmashauri, mikoa pamoja na wizara katika juhudi za kupambana na ueneaji wa kipindupindu kwa kuzingatia yafuatayo:
kunywa maji yaliyo safi na salama
kuepuka kula chakula kilichoandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama
kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka.
kutumia vyoo wakati wote na kutokujisaidia ovyo katika vyanzo vya maji vya mito, maziwa na mabwawa.
Kutokutiririsha maji taka na vinyesi ili kuepuka uchafuzi wa vyanzo vya maji
Pia wananchi wanahimizwa kuwahi mapema katika vituo vya kutolea huduma za afya mara waonapo dalili kuu za ugonjwa wa kipindupindu ambazo ni pamoja na kuanza ghafla kuharisha mfululizo kinyesi cha majimaji na kunako weza kuambatana na kutapika, kulegea, kusikia kiu, midomo kukauka, na kuishiwa nguvu. Mgonjwa anaweza kupoteza maisha endapo hatapata huduma yoyote ya tiba katika muda mfupi na hasa kutokana na kuishiwa maji.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Wizara pia inapenda kuwajulisha wananchi wote kwa ujumla kuhusu juhudi ambazo serikali imezichukua kama hatua za awali za kujiandaa kuzuia maambukizo ya ugonjwa wa homa ya Zika ambao Mheshimiwa Ummy A. Mwalimu (Mb), Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto alishautolea taarifa hapo awali. Wizara imeanza kutekeleza mikakati mbalimbali ya kusaidia kuiweka nchi katika hali ya utayari kupambana na tishio la ugonjwa wa homa ya Zika, Mikakati hiyo ni pamoja na:
Kuimarisha ufuatiliaji wa utambuzi wa watoto waliozaliwa na vichwa vidogo (microcephaly) kupitia hospitali zote za Rufaa kwa kutumia mfumo wa ufuatiliaji wa ugonjwa wa Rubella ambayo inaendelea. Aidha takwimu za watoto waliozaliwa na vichwa vidogo ambazo zimekwisha kukusanywa kwa kupitia mfumo huu zinaendelea kuchambuliwa kwa uhakika ili kuona kama lipo tishio la ongezeko la ulemavu wa aina hii nchini.
Sampuli za wagonjwa wanaojitokeza na homa na kukidhi vigezo vya Zika Virus wanaotolewa taarifa na mfumo huu zitakusanywa na kupimwa katika maabara zilizopo kwenye kituo cha utafiti kilichopo KCMC Moshi “KCRI”.
Kufanya uchunguzi kwa mbu waliokusanywa wakati wa Dengue na kuona iwapo wana virusi hivyo na pia kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa yaambukizwayo na mbu kwa ujumla (Entomological Surveillance) ili kuweza kuiwezesha Serikali kutambua kama kuna viashiria vya virusi hivyo kuwepo katika jamii ya mbu.
Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa kwa baadhi ya maeneo yenye kuwa na wagonjwa wa homa (Acute Febrile Illness Sentinel Surveillance) ili kubaini kama virusi hawa ni sehemu ya vimelea vinavyowasababishia homa au la.
Mwisho Wizara inaandaa Mpango kazi wa namna ya kukabiliana na Zika ambao utakamilika katika kipindi cha wiki moja ijayo.
Hitimisho
Wizara inaendelea kutoa rai kwa jamii, wataalamu na viongozi katika ngazi zote kwamba kila mmoja wetu atimize wajibu wake katika harakati za kuudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu.
Kwa mara nyingine tena tunaendelea kuwashukuru wadau wote, yakiwemo Mashirika ya Kimataifa kwa mchango wao mkubwa katika jitihada zetu za kupambana na magonjwa. Aidha tunawashukuru na kuwapongeza watumishi wa afya katika ngazi mbali mbali kwa juhudi zao katika kupambana na ugonjwa huu. Pia tunawapongeza waandishi wa habari kwa kuendelea kuisaidia Serikali kuielimisha jamii jinsi ya kujikinga na kipindupindu kusambaza taarifa mbalimbali zinazotolewa na Wizara yangu kwa ngazi zote zinazohusika kwenye mapambano ya Kipindupindu
Nawashukuru kwa kunisikiliza
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment