WAZIRI
wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud
Mohamed amemtaka Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kutoa taarifa za
kuwapo kwa tishio la kundi la al Qaeda kuingia nchini kwa vyombo vya
ulinzi na usalama ili vyombo hivyo, vishughulikie hatari hiyo.
Aboud
amesema kwa kuwa Lowassa anaelewa madhara ya ugaidi na ana taarifa za
kina kuhusu kundi hilo, ni vyema akazipeleka kwenye vyombo vya usalama.
“Kuna
nchi za jirani ambazo zimekumbwa na madhara ya ugaidi, sasa kama kuna
watu kama akina Lowassa na wengine wenye maono kama hayo au kuwa na
taarifa za ziada za magaidi basi wapeleke Jeshi la Polisi ili zifanyiwe
kazi,” alisema Aboud
Mwishoni
mwa wiki, Lowassa ambaye alikuwa mgombea urais kupitia Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana,
alionya kuwa ipo hatari Zanzibar ikatumiwa kuwa njia ya kuingia magaidi
wa aina ya Al-Qaeda nchini.
Lowassa
alidai kuwa hilo linaweza kufanyika, endapo jitihada maalumu
hazitafanyika sasa katika kumaliza mkwamo wa kisiasa visiwani humo na
kuzuia uwezekano wa kuvunjika kwa hali ya amani.
Lakini,
Waziri Aboud aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
katika Serikali ya Awamu ya Nne, alisisitiza kuwa Zanzibar ina amani na
utulivu na kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imejipanga
kuhakikisha hali ya utulivu na amani inaendelea kudumu.
“Kama
serikali kupitia vyombo vyake vya usalama, vina utaratibu wake wa
kuhakikisha inashughulikia watu wote wanaofanya uhalifu na vitendo vya
uvunjifu wa amani kwa mujibu wa taratibu za nchi,” alieleza.
Alisema
SMZ itahakikisha inatekeleza agizo la Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)
la kufanyia uchaguzi wa marudio na kuwapo kwa vitisho kutoka kwa baadhi
ya vyama vya upinzani.
“Tutatekeleza
agizo la Tume ya Uchaguzi (ZEC) na niwahakikishie wananchi kuwa
Zanzibar itaendelea kuwa na amani na utulivu kuanzia sasa, wakati wa
kupiga kura na baada ya kupiga kura na kupokea matokeo,” alibainisha.
Zanzibar
inatarajia kufanya uchaguzi wa marudio wa kuchagua Rais wa Zanzibar,
Wawakilishi na Madiwani Machi 20, mwaka huu, baada ya ule uliofanyika
Oktoba 25, mwaka jana kufutwa siku tatu baadaye kwa tangazo la
Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha kutokana na kuwapo kwa kasoro
kadhaa.
Post a Comment