WAZIRI
wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango amesema hatua ya Serikali ya
kukusanya kodi kwa nguvu kwa baadhi ya wafanyabiashara waliotorosha
makontena bila kulipiwa ushuru, haikuwa lengo la kumkomoa mtu, bali
ililenga kukusanya fedha za Serikali yenye lengo la kuifanya nchi iache
utegemezi wa wahisani.
Waziri
huyo ambaye jana alikutana na makundi mbalimbali ya wafanyabiashara
ofisini kwake Dar es Salaam, alisema yeye kama waziri wa fedha
asingependa kuwa waziri ombaomba kwa wahisani, ambao alidai baadhi yao
wana masharti magumu, ambayo hayatekelezeki kwa maadili ya Watanzania.
“Nimewasindikiza
wenzangu huko nje kuomba fedha sasa nimechoka, nataka kutembea kifua
mbele, maana wana masharti magumu, wengine wanataka turuhusu homosexual
(ndoa za jinsia moja), masharti haya kwa kweli yanakera sana,” alisema Dk Mpango ambaye katika serikali iliyopita alikuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango.
Dk
Mpango aliongeza kuwa ili nchi isonge mbele, ni lazima ikusanye kodi ya
kutosha; na jana aliahidi kuchukua hatua kadhaa, zitakazoiwezesha sekta
binafsi kuwa mhimili wa kuimarisha uchumi wa nchi ili kufikia malengo
ya kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye kipato cha kati.
Alisema
Rais John Magufuli ni kiongozi ambaye akilala na kuamka, anawaza namna
ambavyo atawahudumia wananchi wake, ambao wengi wako kwenye dimbwi la
umaskini.
Alisema Rais atafanikiwa tu, pale Serikali yake itakusanya kodi ya kutosha na kuwahudumia wananchi hao.
“Kuna
minong’ono kwamba eti Serikali ya Awamu ya Tano inawanyanyasa
wafanyabiashara wakubwa na kwamba hatua tulizochukua kukusanya kodi,
ililenga kuwadhalilisha baadhi ya wafanyabiashara, hii sio kweli
kabisa,” alisema Dk Mpango.
Dk
Mpango alisema Serikali ya Awamu ya Tano, inatambua umuhimu wa
wafanyabiashara, hivyo wizara yake itakuwa ya mwisho kuchukua hatua za
kuwanyanyasa.
“Nawahakikishia
kwamba nina dhamira ya dhati ya kufanya kazi kwa kushirikiana na ninyi
wafanyabiashara wakubwa na wadogo ili tutimize ndoto ya Rais,” alisema.
Alisema
serikali yoyote duniani ni lazima ikusanye kodi, hivyo aliwahakikishia
wafanyabiashara hao kuwa kama bado kuna wafanyabiashara wanaokwepa au
hawataki kulipa kodi kwa mujibu wa sheria, serikali haitakuwa tayari
kuwavumilia.
Dk
Mpango alisema idadi ya watu wanaolipa kodi kwa sasa nchini bado
wachache, hivyo aliwaagiza wafanyabiashara wote kujisajili wapatiwe
Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN).
Pia,
aliwataka waache tabia ya kufanya udanganyifu kwa kuwa na vitabu vingi
vya utunzaji wa kumbukumbu za biashara. Aliwaagiza kuhakikisha wanatoa
stakabadhi na suala hilo lisiwe hiyari.
“Tunajua kwamba mnatoa vitisho kwa wanunuzi kuwa kama wanataka risiti bei ni ya juu, hiki mnachofanya ni hatari kwa nchi,” alisema na kuwataka wote watumie mashine za EFD na serikali inaendelea na mpango wa kununua zingine ili wagawiwe bure.
Aliwataka
kutoa taarifa kwa Kamishna Mkuu wa TRA, kama kuna mfanyakazi wa Mamlaka
ya Mapato (TRA) au wa Halmashauri ya Wilaya, ambaye atadai hongo au
atawanyanyasa wakati wa kudai kodi.
Katika kutekeleza hilo, aliwapatia namba zake pamoja na za Kamishna na kuwataka waache tabia ya kutoa rushwa ili wasilipe kodi.
Dk
Mpango alisema baada ya wafanyabiashara kufanya kikao na Rais Magufuli,
Serikali imeunda kikosi kazi kushughulikia kero zote, zilizotolewa na
Baraza la Biashara na mojawapo ni kufuta utiriri wa kodi ili kuwapa
wepesi wawekezaji kufanya biashara nchini na kumpungumzia mzigo mkulima.
Post a Comment