Baadhi
ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) waliokumbwa
na ‘operesheni tumbua majipu’, walikutwa na mali nyingi “kupita
maelezo”, kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga.
Operesheni
hiyo, ambayo inatekelezwa tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya
Awamu ya Tano, juzi ilimkumba Dickson Maimu, ambaye alikuwa Mkurugenzi
Mtendaji wa Nida, Joseph Makani (Mkurugenzi wa Tehama), Rahel Mapande
(Ofisa Ugavi Mkuu), Sabrina Nyoni (Mkurugenzi wa Sheria) na George
Ntalima ambaye ni Ofisa Usafirishaji.
Waziri
wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alisema hatua ya kutengua na
kusimamisha watumishi hao imechukuliwa baada ya uchunguzi wa hali ya juu
kwenye mamlaka hiyo.
Ingawa
hakutana kuingia kwa undani akihofia kuingilia uchunguzi, Kitwanga
alisema katika uchunguzi wao, moja ya hatua ilikuwa ni kukamata mali za
wafanyakazi hao wa Nida.
“Walipoulizwa,
walisema wamepata mali hizo kutokana na mikopo, hivyo uchunguzi
utajielekeza katika kulinganisha kiwango cha mikopo na mali walizonazo,”
alisema.
Waziri
huyo alisema uchunguzi zaidi unajielekeza katika ni jinsi gani Sh180
bilioni zilitumika kusajili watu milioni sita tu na kati yao kuwapata
vitambulisho watu milioni 2.5 tu.
“Ninayo
taarifa niliyopewa na Nida ikionyesha kwamba imepanga ofisi nyingi Dar
es Salaam zisizo na matumizi na wakati fulani walinunua ‘seva’ 100
zisizo na matumizi,” alisema.
“Haielezeki,
NEC ilitumia kiasi kama hicho kuandikisha watu milioni 20 katika miezi
isiyozidi mitano, lakini Nida wametumia Sh180 bilioni kuandikisha watu
milioni 2.5 kwa miaka mitatu.”
Mbali
na kuwaweka kando watendaji hao, Rais aliagiza vyombo mbalimbali
kufanya uchunguzi wa matumizi ya fedha katika mamlaka hiyo.
Vyombo
vilivyoagizwa ni pamoja na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa
(Takukuru), Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na
Mamlaka ya Udhibiti ya Ununuzi ya Umma (PPRA).
Post a Comment