Askofu
Cletus Chandrasiri Perera, mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Sri Lanka anasema, maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu
Kimataifa Jimbo kuu la Cebu, Ufilippini ni fursa ya kuadhimisha,
kuabudu, kutafakari na kuzama katika katekesi za kina zinazotolewa
wakati huu wa kongamano, ili kuwawezesha waamini kuonja na hatimaye,
kushuhudia utajiri mkubwa unaofumbatwa katika Fumbo la Ekaristi
Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.
Waamini wanapaswa
kutambua umuhimu wa Fumbo la Ekaristi katika maisha yao, tayari
kulipatia kipaumbele cha kwanza katika maisha yao ya kila siku, ili
kuweza kuipokea na kuimwilisha katika uhalisia wa maisha yao, ili
kushuhudia huruma, upendo na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na
Kanisa lake. Wakati huu, Kanisa Katoliki linaungana kwa pamoja kusali,
kutafakari na kumwabudu Yesu Kristo ambaye daima yuko kati kati ya watu
wake kwa njia ya Neno na Sakramenti, lakini zaidi kwa njia ya maskini,
ambao kimsingi ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu.
Maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu kimataifa
yanajikita katika Ibada ya Misa takatifu,Sala, Katekesi, Tafakari, Ibada
ya Kuabudu na Maandamano la Ekaristi Takatifu ushuhuda wa imani ya
Kanisa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, kielelezo cha uwepo endelevu
wa Kristo kati ya waja wake pamoja na mikutano mbali mbali ya kiimani.
Inafurahisha kuona kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameridhia
maadhimisho ya Kongamano hili yafanyike nchini Ufilippini, nchi ambayo
ina idadi kubwa ya waamini wa Kanisa Katoliki, watu ambao wako moto moto
katika ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, ikilinganishwa
na nchi nyingine kutoka Barani Asia.
Maadhimisho haya ni mkusanyiko wa waamini kutoka sehemu mbali mbali
za dunia wanaoshuhudia umoja na utofauti wao katika imani na upendo.
Wote hawa wanaungana kwa pamoja ili kumwomba Kristo Yesu awaongoze na
kuwaimarisha katika imani inayoshuhudiwa katika matendo ya huruma:
kiroho na kimwili. Ekaristi takatifu ni kiini na hitimisho la maisha na
utume wa Kanisa, kama ambavyo wanakaza kusema Mababa wa Mtaguso mkuu wa
Pili wa Vatican.
Maadhimisho haya ni wakati muafaka kwa Wakristo kutoka Sri Lanka
waliohamia nchini Ufilippini kuweza kukutana na kusali kwa pamoja, ili
kushuhudia imani yao katika Fumbo la Ekaristi Takatifu anasema Askofu
Cletus Chadrasiri Perera, mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Sri
Lanka kwenye maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu
Kimataifa linaloendelea huko Jimbo kuu la Cebu, Ufilippini.
Post a Comment