BREAKING NEWS

Wednesday, 27 January 2016

Mchango wa Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa watawa


Padre Antonio Spadaro, mkurugenzi mkuu wa Jarida maarufu la “Civilta Cattolica” hivi karibuni, amechapisha na kuhariri kitabu ambacho ni mkusanyiko wa mazungumzo yaliyofanywa na Baba Mtakatifu Francisko na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume, baada ya kuhitimisha mkutano wao wa 82 na hapo likazuka wazo la maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani. Kitabu hiki kinaunganisha pia mchango wa Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maisha ya Kuwekwa wakfu, iliyoitishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II na kuadhimishwa kunako mwaka 1994.
Kitabu hiki ni mchango mkubwa unaonesha mahusiano ya Baba Mtakatifu Francisko na Watawa hususan wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani. Haya ni matunda ya majadiliano kati ya Baba Mtakatifu na wakuu wa Mashirika ambao kwa pamoja waliangalia: fursa, changamoto na matatizo yanayowasibu watawa wanapotekeleza dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa. Watawa wanafanya kazi katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, wenye changamoto nyingi.
Kitabu hiki ni msaada mkubwa kwa watawa kufanya tafakari ya kina kuhusiana na wito na maisha yao katika nyakati hizi. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawataka watawa wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kuhakikisha kwamba, wanamwilisha na kuendeleza karama za mashirika yao kwenye Makanisa mahalia, tayari kusoma alama za nyakati, ili kujibu kilio cha watu wa nyakati hizi kadiri ya karama za mashirika ya kitawa.
Baba Mtakatifu anawataka watawa kuwa wasikivu, wadadisi na wagunduzi, daima wakitambua kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa, kumbe wanapaswa kushiriki katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji katika Makanisa mahalia, wakitambua kwamba, wao pia ni sehemu ya Familia ya Mungu inayosafiri kuelekea katika utimilifu na utakatifu wa maisha. Hapa watawa wanahamasishwa kuwa kweli ni waaminifu kwa Mungu na Kanisa.
Watawa wanakabiliwa na changamoto mbali mbali, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa idadi ya miito na ongezeko la wazee na wagonjwa katika Mashirika. Hapa watawa hawana sababu ya kukata wala kukatishwa tamaa, bali wanapaswa kuwa ni mashuhuda na manabii wa nyakati hizi, tayari kuyaangazia maisha ya mwanadamu kwa sasa na kesho iliyo bora zaidi, dhamana inayotekelezwa kwa njia ya huduma makini.
Hapa Kanisa halina budi kufungua malango, tayari kutoka ili kuwaendea maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, tayari kuwaonjesha Injili ya Furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kutoka kwa watawa. Baba Mtakatifu anasema, bila ushuhuda wenye mvuto, Mashirika ya kitawa yatakabiliwa na changamoto kubwa zitakazowakatisha na kuwavunja moyo. Watawa wajenge utamaduni wa kusikiliza na kujibu kilio cha mahangaiko ya watu wanaowazunguka.
Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 1994 alishiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi ya Maisha ya kuwekwa wakfu iliyoitishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II. Katika maadhimisho haya aliwashirikisha Mababa wa Sinodi, kuhusu uzoefu, mang’amuzi na maisha yake kama mtawa na Askofu kwa kuwataka Mababa wa Sinodi kuhakikisha kwamba, maisha na wito wa kitawa unakuwa ni sehemu muhimu ya Familia ya Mungu.
Kamwe watawa wasitengwe wala kubezwa kwani wanachangia kwa kiasi kikubwa katika maisha na utume wa Kanisa, hususan katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima. Watawa wahakikishe kwamba, wanamwilisha karama za mashirika yao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Makanisa mahalia. Hii inatokana na ukweli kwamba, katika historia ya maisha na utume wa Kanisa, kumekuwepo na migogoro kati ya Maaskofu mahalia na Mashirika ya kitawa, kiasi hata cha “kununiana au kuangaliana kwa jicho la makengeza”, kana kwamba watawa ni watu wa kuja!
Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani yasaidie kujenga utamaduni wa majadiliano kati ya Maaskofu mahalia na Mashirika ya kitawa, tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha unaomwilishwa katika huduma ya haki, amani, mapendo na mshikamano wa dhati.
Padre Antonio Spadaro anasema majadiliano kati ya Baba Mtakatifu Francisko na wakuu wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume yanaonesha mwelekeo wa Kanisa kuhusu: maisha, wito na utume wa watawa ndani ya Kanisa. Ni mazungumzo ambayo yalijikita katika uhalisia wa maisha; katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya kuanza mchakato wa majadiliano kati ya viongozi wa Kanisa na Mashirika ya kitawa, ili kweli yaweze kutekeleza wajibu na dhamana yao kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu. Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani ni nafasi ya kuangalia fursa, changamoto na matatizo yaliyopo ili yaweze kufanyiwa kazi kwa kujikita katika ari na mwamko wa kimissionari, tayari kuwatangazia watu wa Mataifa Injili ya Furaha inayojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree