Gazeti la The New York Times la nchini Marekani limefichua ripoti
ya ushirikiano wa kiintelijensia uliopo kati ya Shirika la Kijasusi la
Marekani CIA na Saudi Arabia katika kuibua mgogoro nchini Syria, ripoti
ambayo kwa mara nyingine tena inathibitisha ukweli huu kwamba mgogoro wa
nchi hiyo ya Kiarabu (Syria) umetokana na njama za kigeni.
New York Times ilifichua ripoti hiyo Jumamosi iliyopia kupitia toleo
lake la mtandaoni ambapo sanjari na kuweka wazi taarifa za
kiintelejensia za viongozi wa Marekani na Kiarabu katika baadhi ya nchi
za Ghuba ya Uajemi, limeandika kuwa mwaka 2013 Rais Barack Obama alitoa
amri ya siri kwa shirika hilo la kijasusi la Marekani CIA ili kuwapatia
msaada magaidi wanaopigana dhidi ya serikali ya Syria. Aidha gazeti hilo
limesisitiza kuwa, CIA ilifahamu kuwa ili kutekeleza suala hilo
hakukuwepo mshirika bora zaidi ambaye angeweza kutekeleza suala hilo
kuliko Saudia. Limeongeza kuwa, mpango huo ulitekelezwa na Bandar bin
Sultan, mkuu wa wakati huo wa shirika la ujasusi la Saudia ambaye naye
alitoa amri ya kununuliwa maelfu ya silaha zikiwemo bunduki aina ya
Kalashnikov kwa ajili ya magaidi hao wa Syria. Katika fremu hiyo mkuu wa
Shirika la Kijasusi la Marekani CIA aliiandalia Saudia mazingira mazuri
kwa ajili ya kufanikisha mkataba kabambe wa ununuzi wa silaha kutoka
Croatia. Likiashiria kuwa baada ya hapo ushirikiano baina ya CIA na
shirika la ujasusi la Saudia ulianza kunawiri zaidi, Gazeti la The New
York Times limebaini kuwa, ushirikiano wa Riyadh na shirika hilo la
Marekani, unajiri katika fremu ya mahusiano mazuri ambayo yamekuwepo
baina ya pande hizo mbili kwa miongo kadhaa sasa. Kile kinachotekelezwa
na madola ya Magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu katika kukabiliana
na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, kinajiri katika hali ambayo
kundi hilo limeonyeshwa taa ya kijani na kuongozwa katika jinai zake na
mashirika makubwa ya kijasusi sanjari na kufadhiliwa kwa fedha na silaha
na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na lile la utawala haramu wa
Kizayuni wa Israel (MOSAD) kwa kushirikiana na idara ya usalama ya
Saudia huko nchini Syria. Kundi la Daesh lililo na hamu kubwa ya kufanya
jinai na mauaji ya kutisha katika ngazi ya kieneo na kimataifa, ndilo
lile lile kinaloliundwa na Marekani, Israel na Saudia, ambao ni waungaji
mkono wake wa jadi. Hii ni katika hali ambayo karibu miaka mitano
inapita tangu kulipoanzishwa harakati za kundi hilo kwa lengo la
kuiondoa madarakani serikali halali ya Rais Bashar al-Assad wa Syria,
harakati ambazo hadi sasa zimeshindwa kufikia malengo yaliyokusidiwa.
Ukweli ni kwamba kundi la Daesh ambalo tangu awali limekuwa likitumikia
malengo ya madola ya Magharibi katika kumuondoa madarakani Rais Bashar
al-Assad, sasa limegeuka na kuwa tishio kwa waungaji mkono wake, baada
ya kushindwa kutekeleza kikamilifu mpango wa mabwana zake. Tangu mwezi
Machi mwaka 2011 madola ya Magharibi na Kiarabu katika kujaribu
kumuondoa madarakani rais huyo wa Syria, yamekuwa yakibuni magenge
tofauti ya kigaidi ili kufikia malengo yao haramu katika eneo. Hata
hivyo jinai za makundi hayo hususan Daesh, zimevuka mipaka ya kijografia
nchini Syria na kuzifikia hata nchi zenyewe za Magharibi na hivyo
kuibua wimbi la machafuko katika nchi hizo.
Post a Comment