Kongamano
la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa ni sehemu ya maadhimisho ya Mwaka
Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Kanisa kuangalia kwa namna
ya pekee juu ya Fumbo la Ekaristi Takatifu: chanzo na lengo la maisha na
utume wa Kanisa. Kongamano hili limefunguliwa rasmi tarehe 25 Januari
na litahitimishwa tarehe 31 Januari 2016. Katika maadhimisho ya Fumbo
la Ekaristi Takatifu kazi ya ukombozi iliyo tekelezwa na Kristo Yesu
inadhihirika sanjari na kuonesha uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu
wake.
Mababa wa Kanisa
wanakumbusha kwamba, Ekaristi Takatifu ni chanzo na lengo la maisha na
utume wa Kanisha. Hii ni Sakramenti ya upendo, alama ya umoja na
mshikamano wa dhati na dhamana ya ukarimu kwa maskini na wote
wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Maadhimisho haya yanafanyika Barani
Asia kama nafasi ya kutafakari kuhusu maisha na utume wa Kanisa Barani
Asia unaopaswa kujikita katika majadiliano ya kidini, kitamaduni na
maskini.
Kanisa linapenda kukuza na kudumisha utume miongoni mwa vijana wa
kizazi kipya, kwani Kanisa linatambua kwamba, vijana ni udongo wenye
rutuba nzuri katika maisha na utume wa Kanisa. Ili vijana waweze
kutekeleza vyema dhamana na utume wao, wanapaswa kupewa malezi bora na
endelevu. Mababa wa Kanisa wanatambua nafasi na mchango wa Bikira Maria
katika maisha na utume wa Kanisa. Bikira Maria ni Tabernakulo ya kwanza
ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Kumbe, Bikira Maria ni mfano na
Mama wa Kanisa. Huu ni mwaliko wa kujifunza kutoka katika shule ya
Bikira Maria ili Kanisa liweze kujikita zaidi katika mchakato wa
Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda, ari na mwamko wa
kimissionari.
Waamini wanakumbushwa kwamba, Kristo ndani wao, tumaini la utukufu.
Hii ni mbegu ya Umissionari inayoshuhudia utukufu wa Mungu unaofumbatwa
katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Huu
ndio ushuhuda endelevu wa utukufu wa Mungu ambao unajionesha kwa mtu
mzima na kwamba, maisha ya binadamu ni taswira ya Mungu. Upendo na
huruma ya Mungu inawakumbatia na kuwaambata binadamu wote.
Kardinali Charles Maung Bo, Mwakilishi wa Baba Mtakatifu Francisko
katika maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa
katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya ufunguzi
wa maadhimisho haya anasema, dunia iko kwenye mapambano makubwa dhidi
ya umaskini, magonjwa na baa la njaa duniani. Ni mapambano yanayolenga
kuwapatia watoto heshima na hadhi yao kwa kuwapatia chakula na malezi
bora badala ya Makampuni ya Kimataifa kujikita katika uzalishaji na
usambazaji wa silaha zinazopandikiza utamaduni wa kifo dhidi ya Injili
ya uhai.
Kardinali Maung Bo anawataka waamini pamoja na watu wote wenye
mapenzi mema kusimama kidete, kulinda, kutetea na kushuhudia haki jamii
ikitekelezwa kwa dhati sanjari na kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili
ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa
njia ya matendo ya huruma yanayotiliwa mkazo na Baba Mtakatifu Francisko
wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya
Mungu.
Kardinali Charles Maung Bo anakaza kusema, takwimu za UNICEF
zinaonesha kwamba, kuna idadi kubwa ya watoto wanaopoteza maisha yao
kila siku kutokana na utapiamlo wa kutisha, hali ambayo inaweza
kuonekana kuwa kama ni mauaji ya kimbari. Ulimwengu wa leo unakabiliwa
na changamoto ya ukosefu wa usawa katika mapambano dhidi ya baa la
umaskini duniani. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni
changamoto kwa waamini kuambata haki jamii, kwani kuna uhusiano mkubwa
kati ya Ekaristi Takatifu na umaskini.
Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yanampatia mwamini hadhi na
utu unaomwezesha kushiriki Mkate wa uzima wa milele, Kristo Yesu
aliyeshuka kutoka mbinguni ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi
la dhambi na mauti. Hapa waamini wanapaswa kuwa ni Ekaristi kwa jirani
zao kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa
kifo unaojikita katika sera za utoaji mimba na kifo laini au eutanasia.
Waamini wanayo Ibada kubwa kwa Ekaristi Takatifu, lakini haitoshi
anakaza kusema Kardinali Charles Maung Bo, kwani Kristo anawataka
wafuasi wake kumfuasa kwa kubeba Misalaba yao; tayari kujisadaka katika
mapambano dhidi ya umaskini; unyonyaji, udhalimu, ukandamizaji na badala
yake kujenga mshikamano wa upendo na huruma kwa kujitahidi kumwilisha
matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama anavyokazia Baba Mtakatifu
Francisko wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya
huruma ya Mungu.
Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya ufunguzi wa Kongamano la 51 la
Ekaristi Takatifu Kimataifa limehudhuriwa na viongozi wengi wa Kanisa
pamoja na familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Ufilippini.
Maadhimisho haya yanayongozwa na kauli mbiu “Kristo ndani yenu, tumaini
letu la utukufu”.
Post a Comment