Tume ya Huduma za Mahakama Kenya JSC
imeteua jopo la maafisa 6 kuchunguza tuhuma za ulaji rushwa ya zaidi ya
dola milioni 2 zinazomkabili jaji wa mahakama ya juu nchini humo Philip
Tunoi.
Rais wa tume hiyo ambaye pia ni Jaji mkuu Dkt Willy
Mutunga ametangaza hayo baada ya kikao maalum cha dharura kilichoitishwa kufuatia hatua ya Bw Geoffrey Kiplagat kupasua mbarika kuwa yeye ndiye aliyefanikisha hongo ya dola milioni mbili kwa jaji Tunoi ili awashawishi wenzake kupendelea upande mmoja wakati wa uamuzi wa kesi ya kupinga uchaguzi wa gavana wa jimbo la Nairobi Dkt Evans Kidero.
Jopo hilo linajumuisha mkuu wa sheria Prof Githu Muigai, Mkuu wa tume ya utumishi wa umma Prof Margaret Kobia, jaji Aggrey Muchelule, Bi Emily Ominde, Bi Winnie Guchu na Bw Kipkorir Bett.
Sita hao wanapaswa kukamilisha uchunguzi huo na kutoa taarifa kwa tume hiyo inayosimamia maswala ya haki na mahakama nchini Kenya katika kipindi cha siku saba sijazo.
Jaji Phillip Tunoi amejitokeza wazi wazi na kukanusha tuhuma hizo kwamba alipokea hongo kutoka kwa gavana wa Nairobi Kidero.
Gavana huyo pia amekanusha madai yoyote dhidi yake akisisitiza kuwa ushindi wake ulikuwa huru na wa haki.
Aidha wawili hao wamekanusha kuwa wanamjua Bw Kiplagat na kusema kamwe hawajawahi kukutana naye
Jaji Tunoi anadai kuwa madai na tuhuma zinazomkabili sio ya kweli na kudai kuwa hiyo ni njama ya kumng'oa katika mstari wa mbele wa kuwania nafasi ya kuongoza jopo la majaji wa mahakama ya juu zaidi nchini Kenya.
Mahakama hiyo iligonga vichwa vya habari mwaka 2013 ilipotoa uamuzi uliothibitisha kuwa rais Uhuru Kenyatta alikuwa amemshinda mpinzani wake wa karibu Raila Odinga katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka wa 2013.
Tunoi anasema uwezekano wa kuamua ni nani atakayeiongoza Kenya baada ya uchaguzi ujao wa 2017 ndio uliozua mchecheto miongoni mwa wahusika ambao wanashuku kuwa msimamo wake thabiti hautapendelea mwanasiasa wanaomuunga mkono.
Hata hivyo Jaji Tunoi amekariri kuwa hatachelea hata kwa sekunde moja kufunganya virago vyake iwapo Bw Kiplagat anayemtuhumu kwa kupokea hongo hiyo kubwa atatoa chembe moja ya ushahidi dhidi yake.
Jaji huyo kwa sasa anaendelea na kesi ambayo anapinga kustaafishwa kwake kwa lazima baada ya kutimiza miaka 70 kwa mujibu wa katiba ya Kenya.
Tunoi pamoja na majaji wengine wakongwe wanadai kuwa wanapaswa kuruhusiwa kustaafu wakitimiza miaka 74 kwa mujibu wa katiba ya zamani.
Post a Comment