BREAKING NEWS

Wednesday, 27 January 2016

Andrew Chenge Achaguliwa Kuwa Mwenyekiti wa Bunge.....Asema Suala La Escrow Likirudi Bungeni Atakaa Pembeni


MBUNGE wa Bariadi, Andrew Chenge na wabunge wawili wa Viti Maalumu, Dk Mary Mwanjelwa na Najma Giga, wamechaguliwa kuwa Wenyeviti wa Bunge kwa kipindi cha miaka miwili na nusu.

Uchaguzi huo ulifanyika jana baada ya majina yao kupendekezwa na Kamati ya Uongozi na kuyawasilisha bungeni kwa ajili ya uchaguzi.
 Katika uchaguzi huo, uliotanguliwa na wabunge hao kujieleza mbele ya wenzao na kuulizwa maswali, sakata la Tegeta Escrow liliibuka baada ya Chenge kujieleza.

“Katika Bunge lililopita, chama chako na wabunge walikuwajibisha kwa kashfa ya Escrow, je, siku ukiliongoza Bunge na hoja ikarudi ndani uko tayari kuisimamia,” Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe (Chadema) alimuuliza Chenge.

Akijibu swali hilo, Chenge alisema Bunge linaongozwa na Kanuni na itakapokuja mbele ya Bunge au kwenye Kamati, ikaonekana kuna maslahi ama inamhusu mbunge, ni busara kuzingatia kanuni nafasi hiyo ikaachwa mwingine aifanye shughuli za Bunge zisiwe na makandokando ya aina yoyote.

“Naona niishie hapo, ningeweza kusema zaidi ya hapo,” alisema Chenge ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa zaidi ya miaka 10 na pia Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la 10 kabla ya kujiuzulu kutokana na sakata la Tegeta Escrow.

Awali akijieleza Chenge ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, alisema “napenda niliahidi Bunge na Watanzania kwa ujumla, kwamba hii ni dhamana nzito ya kumsaidia Spika na Naibu.

“Lakini niwahakikishie nitatekeleza jukumu hilo kwa uadilifu, na kwa uaminifu ili nitende haki inayoonekana na bila chuki, wala upendeleo wowote kwa faida ya kujenga misingi bora ya Bunge hili lakini pia kwa kuwatumikia Watanzania wote,” alisema.

Kuhusu swali la Mbunge wa Nsimbo, Richard Mbogo (CCM) aliyetaka kufahamu ni namna gani Chenge atadhibiti matumizi ya lugha ya kuudhi au kudhalilisha wengine, Chenge alisema Kanuni za Bunge kama zilivyo sheria za nchi, zinakata pande zote kama ilivyo msumeno.

Alisema ikithibitika kwamba mbunge amekiuka kanuni, kiti kitazingatia baada ya kupima kauli na maelezo aliyotoa bungeni.

“Baada ya kupima, tuhakikishe kwamba tunayosema humu bungeni yawe ya kweli, kweli tupu yasiwe ya uongo,” alisisitiza.

Mwanjelwa ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu mkoani Mbeya, katika kujieleza mbele ya wabunge, aliomba wamwamini na kuahidi kuwatumikia bila kujali itikadi kwa faida ya wananchi wote.

Mwanjelwa alikiri kwamba Bunge hili lina changamoto nyingi, lakini atakachozingatia ni utaifa kwanza. 
Najma, ambaye kitaaluma ni Mwanasheria, aliahidi kuwa msaada mkubwa kwa Spika. Aliahidi kuwa atahakikisha anaweka maslahi ya taifa mbele kwa kutoa haki sawa kwa wabunge wote bila kujali vyama vyao.

Spika wa Bunge, Job Ndugai alihoji kwa pamoja wanaoafiki mapendekezo ya Kamati ya Uongozi, ndipo wabunge walio wengi wakaridhia Chenge, Mwanjelwa na Najma wawe wenyeviti. Wenyeviti wa Bunge hufanya kazi wakati ambao Spika au Naibu Spika wakiwa hawapo bungeni.

Katika Bunge la 10, wenyeviti walikuwa Mussa Azzan Zungu, Kidawa Himid Saleh, Lediana Mng’ong’o, Muhammed Seif Khatib, Sylvester Masele na Jenista Mhagama.

Kwa mujibu wa Ndugai, Kamati yau Uongozi imejiwekea utaratibu wa kupendekeza majina na ilipokutana chini ya uenyekiti wa spika, iliamua kuwapendekeza wabunge hao watatu ambao wote ni kutoka CCM.

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree