Mabosi
wa mashirika mawili ya Serikali nchini, wanaodaiwa kulipwa mshahara wa
Sh milioni 36, wamekanusha madai hayo, huku wakielezea kushangazwa na
taarifa hizo wakati hata nusu ya fedha hizo, hawapati.
Akizungumza
mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma
(PIC), mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu alisema halipwi
mshahara huo.
Akijibu
hoja za wajumbe wa kamati hiyo kuhusu taarifa ya utekelezaji na
utendaji wa shirika hilo kwa mwaka 2014/15, Mchechu alisema shirika hilo
pamoja na kutekeleza majukumu yake, bado lina changamoto za uhaba wa
fedha.
“Katika
ujenzi wa nyumba zetu, Serikali haigharamii masuala ya miundombinu kama
vile maji, umeme, barabara hilo ni jukumu letu na linatugharimu fedha
nyingi.
“Sasa
nashangaa wako watu wanasema mimi nalipwa mshahara mkubwa, sielewi
wametoa wapi huo mshahara kwa sababu silipwi mshahara huo, mimi nalipwa
chini ya huo walioutaja,” alisema Mchechu.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za
Nishati na Maji (Ewura),Felix Ngamlagosi aliiambia kamati hiyo kwamba
mamlaka hiyo ina changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa watumishi na maslahi
duni.
Alisema
wakati maslahi ya wafanyakazi ni duni, ameshangaa kusikia vyombo vya
habari vikisema yeye ni miongoni mwa wakurugenzi wanaolipwa Sh milioni
36 kwa mwezi.
“Jamani
hapa tunazungumzia maslahi duni ya watumishi wetu, nashangaa kusikia
naambiwa nalipwa milioni 36, mshahara wangu haufiki hata nusu ya hizo
fedha,” alisema Ngamlagosi.
Nyumba nafuu
Awali
wajumbe wa kamati hiyo baada ya kupitia taarifa hiyo ya NHC, waliiomba
Serikali kuharakisha kuwepo kwa sera ya nyumba ili kurahisishia
mashirika yanayohusika na masuala ya ujenzi wa nyumba kujenga nyumba za
bei nafuu kwa wananchi.
“Yapo
malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba NHC mnauza nyumba kwa bei kubwa,
huku mkitoa matangazo kuwa nyumba hizo ni bei nafuu,” alihoji mjumbe wa Kamati hiyo, Mbunge wa Ushetu, Elias Kwandikwa.
Akijibu
hoja hiyo, Mchechu alisema nyumba zinazojengwa na NHC zinauzwa kuanzia
Sh milioni 30 hadi 250 kwa fedha taslimu na kwamba mnunuzi atatakiwa
kulipa kodi.
Aliongeza
kuwa kama mnunuzi hatakuwa na fedha taslimu, benki washirika wanatoa
mikopo kwa ajili ya ununuzi wa nyumba hizo, ila wanunuzi watatakiwa
kulipa riba za benki husika.
Baada
ya majibu hayo, wajumbe hao walitaka Serikali iangalie jinsi ya
kupunguza mzigo kwa shirika hili na ikiwezekana waondolewe kodi ya
uingizaji vifaa vya ujenzi ili kusaidia nyumba hizo kuuzwa kwa bei
nafuu, kwa lengo la kuwanufaisha wananchi hasa wale wa kima cha chini.
Akizungumzia
hoja hizo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Angelina Mabula alisema shirika hilo, linapaswa kuwasiliana na watendaji
katika maeneo husika ya ujenzi wa nyumba hizo, ili wawasaidie kubeba
gharama ndogondogo.
“Serikali
na wizara zinafanya kazi kwa ushirikiano na NHC, na hili la gharama za
miundombinu, kila halmashauri nchini ambayo ujenzi wa nyumba hizo
unafanywa, inaweza kuangalia jinsi ya kusaidia gharama za miundombinu,
ili nyumba hizo ziuzwe kwa bei nafuu zaidi kwa wananchi,” alisema Mabula.
Post a Comment