WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema tatizo la rushwa barani Afrika
limesababisha bara hilo lipoteze dola za Marekani bilioni 150 kila
mwaka.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Machi 8, 2016) wakati akihutubia
wajumbe wa mkutano wa tano wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA)
linaloendesha vikao vyake jijini Dar es Salaam. Mkutano huo ulioanza
Machi 6, utamalizika Machi 18, mwaka huu.
Akizungumza
kwa niaba ya Rais Dk. John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu alisema rushwa
imechangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya Jumuiya hiyo. "Rushwa
yaweza kuwa kwa njia kuhonga fedha, kupata fedha kwa kula njama,
kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, ama kwa njia za vitisho,"
alisema.
"Kwa
mujibu wa taarifa ya Umoja wa Afrika (AU), rushwa na urasimu
vimeainishwa kuwa ni vikwazo vikubwa vinavyochangia kuchelewesha
ufanyaji wa biashara kwenye mipaka ya nchi za Jumuiya yetu," alisema.
Amesema
sekta binafsi inachukuliwa kama injini ya maendeleo na ukuaji wa uchumi
na akatumia fursa hiyo kuipongeza jumuiya ya wafanyabiashara wa Afrika
Mashariki kwa kuandaa kanuni za kiutendaji ambazo zimelenga kuhamasisha
uadilifu kwenye ufanyaji biashara unaozingatia haki za binadamu, sheria
za kazi, utunzaji mazingira na vita dhidi ya rushwa.
Akizungumzia
kuhusu uondoaji wa vikwazo visivyohusisha kodi (non-tariff barriers)
kama njia mojawapo ya kuimarisha biashara kwenye jumuiya hiyo, Waziri
Mkuu alisema kwa upande wa Tanzania, vizuizi vya barabarani kwenye
barabara kuu ya Kaskazini vimepunguzwa kutoka 50 hadi vitano.
Alivitaja
vizuizi vitano vilivyobakia kuwa ni vile vilivyopo kwenye mizni ya
Mikese (Morogoro), Nala (Dodoma), Njuki (Singida), Mwendakulima
(Shinyanga) na Nyakahura (Kagera).
"Sheria
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya uondoaji wa vikwazo visivyohusisha
kodi ilipitishwa Machi 2015 na sasa hivi inaendelea kusainiwa na Wakuu
wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Pamoja na mambo mengie, nia ya
sheria hii ni kuondoa vikwazo vinavyosababisha uagizaji wa bidhaa kutoka
nje ya nchi na uuzaji wa bidhaa nje ya nchi, kurahisisha sheria za
biashara ndani ya Jumuiya yetu," alisema.
Akizungumzia
kuhusu miradi ya uwekezaji ya Jumuiya hiyo, Waziri Mkuu alisema miradi
ya ujenzi wa barabara inahitaji kiasi cha dola za marekani bilioni 20;
ukarabati na upanuzi wa njia za reli unahitaji dola za marekani bilioni
30; uendeshaji wa mashirika ya ndege na viwanja vya ndege unahitaji dola
za marekani bilioni 15; uendelezaji bandari na usafiri wa majini
unahitaji dola za marekani bilioni 10; utekelezaji wa miundombinu ya
nishati inahitaji dola bilioni 5 ambavyo kwa pamoja vinahitaji dola
marekani bilioni 80.
Alisema
kuwepo kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi ndani ya jumuiya hiyo,
kunaifanya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhesabika kuwa ni jumuiya yenye
nguvu kubwa ya kiuchumi barani Afrika.
Post a Comment