WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amepokea misaada mbalimbali kwa ajili ya wakazi wa vijiji
vya Mtondo na Nanjaru wilayani Ruangwa mkoani Lindi ambao nyumba zao
ziliezuliwa na upepo Januari mwaka huu.
Akizungumza na wananchi wa vijiji hivyo leo (Jumapili, Februari 28, 2016), Waziri Mkuu alisema maafa huwa yanakuja bila kutarajiwa na akatumia fursa hiyo kuwashukuru wadau waliotoa misaada ya chakula, magodoro, mashuka, vitenge, mabati na mbegu za mazao.
Aliwataja wadau hao kuwa ni benki ya NMB, NSSF, wakazi wa Ruangwa na marafiki wa Ruangwa waishio Dar es Salaam ambao walifika kukabidhi misaada hiyo.
Waziri Mkuu ambaye yuko kwenye ziara ya siku mbili katika mikoa ya Mtwara na Lindi kukagua athari za mafuriko, hatua zinzochukuliwa za utoaji misaada kwa waathirika na kuwapa pole wananchi walioathirika na mafuriko hayo, alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi waishio mabondeni wahame kwa sababu mvua kubwa bado zinakuja.
"Jambo
hili si mipango ya mtu binafsi na sote tunajua kwamba tunahitaji mvua kwa ajili
ya mazao lakini safari hii zimekuja zaidi ya kiwango cha kawaida. Mamlaka ya hali
ya hewa imeshasema kuwa mvua kubwa zaidi zinakuja ifikapo Machi mwaka huu",
alisema.
Ili
kuepusha maafa zaidi, kuanzia sasa, wale waliojenga mabondeni wanapaswa wahame.
Pia nawasihi wananchi wachukue tahadhari wakiona mvua inakuja na upepo mkali
wasikae ndani ya nyumba sababu hapa kijijini tumempoteza mzee wetu mmoja ambaye
aliangukiwa na nyumba baada ya nyumba yake kuangukiwa na mti kutokana na mvua
hizo," aliongeza.
Kwa
mujibu taarifa ya maafa iliyotolewa na Mkuu wa wilaya ya Ruangwa, Bi. Mariam
Mtima, mvua zilizonyesha kati ya Januari na Februari mwaka huu zilisababisha nyumba
393 kuezuliwa na nyingine kubomoka na kuacha wakazi wa vijiji hivyo bila
makazi.
"Zahanati
ya kijiji cha Mtondo iliezuliwa paa, daraja la mto Muhuru limebomoka na
halipitiki kabisa na ekari 1,186 za mashamba ya wananchi zimesombwa na maji.
Mazao yaliyoathirika ni mahindi, muhogo, mikorosho, mtama, ufuta, kunde, mpunga
na mbaazi," alisema Mkuu huyo wa wilaya katika taarifa yake.
Alivitaja
vijiji vingine ambavyo mafuriko hayo yaliharibu mashamba ya wananchi kuwa ni
Nambilanje, Mkaranga, Namkatila, Chinongwe A, Likwachu, Nauname na Mbekenyera.
Alisema
hali hiyo imesababisha upungufu mkubwa wa chakula wilayani humo na sasa hivi
wanahitaji tani 1,133 za chakula aina wanga ambazo anataraji zitatosheleza
mahitaji kwa mwezi Machi 2016.
Post a Comment