Monday, 7 March 2016
Watawa waliouwawa huko Yemen ni mashuhuda wa upendo!
Posted by Unknown on 15:00:00 in | Comments : 0
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 6 Machi 2016 alipenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watawa wa Shirika la Wamissionari wa Upendo, maarufu kama Masista wa Mama Theresa wa Calcutta ambao wamegubikwa na msiba mkubwa kutokana na mauaji ya watawa wake wanne, yaliyotokea Ijumaa tarehe 4 Machi 2016 huko Aden, nchini Yemen walikokuwa wanawahudumia wazee. Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwaombea pia wale wote waliouwawa kutokana na shambulizi hili la kigaidi pamoja na familia zao, ili ziweze kuubeba msiba huu mzito kwa imani na matumaini.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, hawa ni mashuhuda wa imani kwa nyakati hizi! Ni watu ambao hawawezi kuwa ni sehemu ya habari inayopewa uzito wa juu; kwa baadhi ya vyombo vya habari, hii si habari! Hawa ni watu wanaoyamimina maisha yao kwa ajili ya utume na maisha ya Kanisa. Ni wahanga wa mashambulizi ya kigaidi na kielelezo cha utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyeheri Mama Theresa wa Calcutta awasindikize watoto wake ambao wamekuwa ni mashuhuda wa upendo kwenye maisha ya uzima wa milele pamoja na kuombea amani na heshima kwa utakatifu wa maisha ya binadamu!
Wakati huo huo, Baba Mtakatifu anasema ameguswa na kufurahishwa na mpango mkakati unaofanywa na Italia kwa kushirikiana na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio pamoja na Makanisa mbali mbali nchini Italia kwa ajili ya kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi. Hawa ni watu wanaokimbia vita, watoto wagonjwa, walemavu, wajane na wazee. Hiki ni kielelezo cha mshikamano wa kiekumene katika kukabiliana na changamoto zinazogusa binadamu wa nyakati hizi. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewasihi waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumkumbuka yeye pamoja na wasaidizi wake wa karibu walioanza mafungo ya maisha ya kiroho kwa kipindi hiki cha Kwaresima, Jumapili jioni, huko Ariccia, nje kidogo ya mji wa Roma.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment