Saturday, 19 March 2016
Sherehe ya Mtakatifu Yosefu!
Posted by Unknown on 20:44:00 in | Comments : 0
Leo Kanisa linaadhimisha Sherehe ya Mtakatifu Yosefu baba mlishi wa Bwana wetu Yesu Kristo na mume wa Mama yetu Bikira Maria. Huyu anaitwa mtumishi mwaminifu wa Mungu. Ni uaminifu wake huo ambao unamshirikisha kwa namna iliyositirika katika historia nzima ya wokovu wetu. Matendo yake ya kiimani hayadhiiriki kwa wazi sana katika maandiko matakatifu lakini ni ya kupewa mkazo wa kipekee mathalani kwa kuwa mtii katika hali ya ukimya wakati wa kuitikia sauti ya Mungu. “Huyu ndiye wakili mwaminifu na mwenye busara”. Maneno haya ndiyo yanafungua ibada ya sherehe ya leo na kutuwekea fadhila mbili muhimu, uaminifu na busara, kama kichocheo katika uwakili wetu au utumishi wetu kwa Mungu. Ni vema basi tukazitafakari fadhila hizi mbili ili kuipata maana kamilifu ya utii wa Mtakatifu Yosefu ambao anautimiliza katika hali ya ukimya.Kama ilivyokuwa kwa Mama yetu Bikira Maria, “ndiyo” yake Mtakatifu Yosefu katika mpango wa Mungu wa ukombozi wa mwanadamu ndiyo inampatia ukuu. Tumesikia katika Injili ya Sherehe hii ya leo: “Naye Yosefu alipoamka usingizini alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza”. Ni mwanzo wa safari ya utii wa Mtakatifu wa Yosefu katika mpango mzima wa ukombozi wa mwanadamu. Yeye kama baba ndani ya familia hii ya Nazareti anayachukua kikamilifu majukumu yake ya kuwa mlinzi na tegemezi kwa familia nzima. Baba Mtakatifu Yohane Paulo II katika waraka wake Redemptoris Custos anaongeza kwa kusema: “Kama vile mtakatifu Yosefu alivyochukua jukumu la kumtunza kwa upendo Bikira Maria na kwa furaha akajitoa katika kumtunza Yesu Kristo, vivyo hivyo ndiyo anavyolitunza na kuliangalia Fumbo la Mwili wa Kristo, Kanisa ambalo Bikira Maria ni mfano na kielelezo”.
Nafasi hii ya Mtakatifu Yosefu inatekelezwa katika hali ya unyenyekevu na ukimya kabisa. Mtakatifu Yosefu anaonesha mfano bora kabisa kwa maisha yetu ya kikristo. Daima hakusita kutimiza wajibu wake kama Baba wa familia. Pia alitimiza wajibu huu kwa uaminifu mkubwa kabisa hata katika mazingira ambayo yalikuwa ni magumu kueleweka. Tunasoma katia Injili jinsi alivyoangaika na Mama yetu Bikira Maria akiwa karibu naye kama mme wake mwaminifu wakati wa kuzaliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Pia alijitoa mhanga kusafiri usiku kucha wakati wakimtorosha mtoto Yesu ili kuilinda familia hii takatifu ya Mungu na mkono dhalimu wa mfalme Herode. Katika maisha ya familia kule Nazareti aliangaika kama Baba kuitafutia familia mahitaji yake ya kila siku na hii inathibitishwa na jinsi Kristo alivyojulikana kuwa ni “Mwana wa Seremala”.
Mtakatifu Yosefu aliyatimiza yote hayo kwa sababu ya ufunuo wa Mungu alioupata kwa njia ya malaika: “Usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uwezo wa Roho Mtakatifu”. Hapa anaiona nafasi ya Mwenyezi Mungu na kwa sababu ya ukubwa wa imani yake anatekeleza yote kadiri ya mapenzi ya Mungu. Ni kielelezo kikubwa anachotupatia katika maisha yetu ya kikristo. Mara nyingi tumefunuliwa juu ya mapenzi ya Mungu katika nyanja mbalimbali za maisha yetu. Wakati mwingine ufunuo huo unatutaka kupitia katika changamoto na mazingira magumu sana. Kwa bahati mbaya sana na kwa sababu ya kuvutwa na mwenendo wa kidunia sauti hii ya Mungu huwekwa kando. Tunakuwa tupo tayari kuitoa sadaka sauti ya Mungu kwa makusudi ya kutaka kusikika na kupata umaarufu.
Changamoto anayokumbana nayo Mtakatifu Yosefu ni kubwa sana kwa kadiri ya mila na desturi za kiyahudi, lakini, kwa kuwa anafunuliwa kuwa kuna mpango wa Mungu ndani mwake anaipokea, anatii na kuitekeleza kwa busara kubwa sana. Hakutoka nje na kuanza kutangaza kwamba ujauzito wa Maria ni kwa uwezo wa Mungu, aliiacha jamii inayomzunguka ielewe kuwa yeye anawajibika kama baba na ndiyo maana alimchukua Maria mkewe na “alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza”. Yeye anakuwa mfano wa Mtumishi mwaminifu tunayemsikia kupitia Nabii Isaya akisema: “Bwana Mungu amenipa ulimi wa hao wafundishwao ... sikio langu lipate kusikia kama wafundishwao ... wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma ... sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate” (Is 50: 5 – 7). Huu ndiyo utii wa kimya kimya ambao tunafundishwa na Kristo kwa ajili ya kuufanya ufalme wa Mungu utawale hapa duniani. Hakika huyu ndiye wakili mwaminifu na mwenye busara.
Somo la kwanza la Sherehe ya leo linafafanua zaidi utii kwa sauti ya Mungu. Mfalme Daudi alitamani kumjengea Mungu nyumba. Alikuwa na uhakika na uwezo wake na ufahari wake lakini Mwenyezi Mungu anayapindua mawazo yake: “Nawe siku zako zitakapotimia, ukalala na baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitaufanya imara ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu”. Mwenyezi Mungu anataka kutufundisha kwamba ni katika kuwa waaminifu na kumtegemea Yeye ndipo tunapoweza kujenga nyumba kwa ajili yake. Hiyo ndiyo nyumba iliyojaa amani, furaha, uelewano, msamaha na katika ujumla wa yote upendo wa kimungu. Ni Mungu mwenyewe ndiye atakayejenga nyumba hiyo kwa mawe yanayothibitishwa na kuimarishwa na Roho wake Mtakatifu.
Mtakatifu Yosefu anapotuonesha utii huu kwa sauti ya Mungu anaendelea kutufundisha kuwa katika hali ya upole na ukimya, katika hali ya unyenyekevu na kujishusha ndipo tunapoweza kupata fursa ya kukaa kimya, kutafakari na kuyaona mambo katika uhalisia wake. Hekima haiji kwa kelele, mabavu na kujitutumua bali ni katika busara hii kubwa tunayojifunza kutoka kwa Mtakatifu Yosefu. Leo hii tunashuhudia familia nyingi zikisambaratika sababu kunakosekana hali hii ya upole na utulivu. Mara nyingi tunafikiri kuwa mtii na mpole ni ubwege. Mmoja ndani ya familia anapokosea tunakosa uwezo wa kumpatia fursa ya kujieleza aidha kwa maneno yake au kwa tafakari zetu katika tendo lake. Matokeo yake hatutoi nafasi ya kuifunua mioyo yetu na kuwa vyombo vya msamaha, yaani kuwa mitume wa Kristo ambao daima wanatafuta kujenga na si kubomoa.
Tunaposherehekea sikukuu hii kubwa nakualika kugutuka na kutoka katika mwendo wa ulimwengu huu unaotuzunguka kwa kelele nyingi na majibu ya haraka haraka. Tujifunze upole na unyenyekevu wa Mtakatifu Yosefu ili kwa njia hiyo tuwe na fursa ya kuutambua mpango wa Mungu na kuupokea hata kama unatupatia changamoto kubwa ya kimaisha. Katika mwaka huu wa Jubilei ya huruma ya Mungu tunampata yeye aliye mfano kwetu wa kuwa vyombo vya kusikilizana na kuchukuliana katika hali ya upole na unyenyekevu. Huyu ni Mtakatifu Yosefu ambaye anatufundisha kwamba ni katika utii wa kimya kimya ndipo tutaweza kuufunua uso wa Mungu mwenye huruma. Nakutakia maadhimisho mema ya Sherehe hii ya Mtakatifu Yosefu.
Mtakatifu Yosefu, Utuombee!
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment