Matukio ya wajawazito kupoteza watoto kwa madai ya uzembe wa wahudumu wa
afya yameendelea kuugubika Mkoa wa Mwanza baada ya mkazi wa Nyarawambo
wilayani Sengerema Tatu Muhangwa, kujifungua na mtoto wake kufariki kwa
kukosa huduma.
Mama mzazi wa Tatu, Vumilia Nailon alisema mjukuu
wake alifariki baada ya wahudumu wa afya katika Zahanati ya Ngoma ‘B’
iliyopo Kata ya Nyamatongo wilayani Sengerema, kuchelewa kumhudumia.
Mhudumu
wa afya aliyekuwa zamu, Helena Mulwisha alisema alishindwa kumhudumia
mjamzito huyo kutokana na kubaini kuwa mtoto alikuwa kakaa vibaya
tumboni na kuwashauri kumpeleka hospitali ya wilaya kwa msaada zaidi.
Nailon
alisema: “Nilimfikisha mgonjwa wangu zahanati juzi, saa kumi na moja
alfajiri, lakini hadi saa tatu hakuwa amepatiwa huduma yoyote hadi
alipojifungua mwenyewe bila msaada na mtoto kufariki.
“Mmoja wa
wahudumu wa afya aliyekuwapo alishindwa kumhudumia baada ya kugundua
mtoto amekaa vibaya tumboni na yeye hana utaalamu wa kumsaidia.”
Alisema
Mulwisha aliwashauri kumpeleka mgonjwa hospitali ya wilaya kwa sababu
wauguzi na madaktari walikuwa wakihudhuria semina.
“Baada ya
kukosa gari ya kumuwaisha hospitali, tuliamua kutembea kwa miguu umbali
wa kilomita mbili, lakini hatukufika baada ya magonjwa wangu
kujifungulia njia kwa msaada wa wasamaria wema na mtoto kufariki,”
alisema Vumilia.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Dk
Henry Nyamete alisema ofisi yake inachunguza tukio hilo na kwamba
itachukua hatua za kinidhamu dhidi ya mhudumu wa afya aliyekuwa zamu
siku hiyo kwa kushindwa kuwajibika kwa kuita gari la wagonjwa ili
kumuwahisha mjamzito huyo hospitali kwa matibabu zaidi.
Post a Comment