Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kuwa sherehe za kuapishwa kwa Rais
mteule wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein zitafanyika siku ya Alhamisi
Machi 24 katika uwanja wa Amaan, na maandalizi yote yamekamilika katika
shughuli hiyo inayotarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo
Rais John Pombe Magufuli pamoja na viongozi wengine wa kitaifa, katika
siku hiyo ambayo pia imetangazwa kuwa ni ya mapumziko kwa upande wa
Zanzibar ili kuwapa fursa wananchi kuhudhuria kwa wingi katika hafla
hiyo.
Tamko
hilo limetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar, Bwana Mohamed Aboud katika mahojiano maalum kuhusiana na
maandalizi ya kuapishwa kwa Rais mteule wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein
ikiwa ni siku chache tangu kutangazwa kuwa mshindi wa nafasi hiyo
katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20 mwaka huu.
Waziri
Aboud amesema mbali na Viongozi wa kitaifa, Mawaziri wa Serikali zote
mbili, Wabunge, Viongozi wa vyama vya upinzani, Mabalozi
wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania, viongozi wa dini na asasi za
kiraia pia wamealikwa katika sherehe hiyo itakayofanyika kuanza asubuhi
na kumalizika saa saba za mchana.
Akizungumzia
kitendawili cha hatma ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Waziri Aboud
amesema kuwa mara baada ya kuapishwa kwa Rais mteule, ataunda Serikali
yake kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar.
Aidha,
Waziri Aboud amewataka wananchi wa Zanzibar hasa wafuasi wa Chama cha
Mapinduzi kuendelea kusherehekea ushindi wao bila ya kumbughudhi mtu
yoyote na kuendelea kudumisha hali ya amani na utulivu visiwani hapa.
Post a Comment