
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa
Jamhuri ya Kenya Mheshimiwa Uhuru Muigai Kenyatta, wameweka jiwe la
msingi katika ujenzi wa barabara ya Arusha - Holili - Taveta - Voi,
yenye urefu wa kilometa 234.3 ambayo inaunganisha nchi za Tanzania na
Kenya.
Hafla ya uwekaji wa jiwe hilo la Msingi imefanyika jana katika eneo la Tengeru Mkoani Arusha na kuhudhuriwa na viongozi wengine wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ni Rais wa Jamhuri ya Uganda Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Makamu wa pili wa Rais wa Jamhuri ya Burundi Dkt. Joseph Butore, Mwakilishi wa Rais Paul Kagame wa Jamhuri ya Rwanda ambaye ni Waziri wa Afrika Mashariki wa Rwanda Mheshimiwa Valentine Rwabiza na Makamu wa Pili wa Rais Sudan Kusini Mheshimiwa James Wan Iga.
Uzinduzi huo pia umehudhuriwa na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein.
Kwa
upande wa Tanzania ujenzi wa barabara hiyo unatakelezwa kwa awamu mbili
ambapo awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka
Arusha hadi Tengeru yenye urefu wa kilometa 14.1, na ujenzi wa barabara
ya mzunguko yaani "Bypass" yenye urefu wa kilometa 42.4.
Awamu
ya pili itahusisha ujenzi wa barabara ya njia nne kuanzia Tengeru hadi
Usa River yenye urefu wa kilometa 8.2 na Kutoka Usa River hadi Holili
mpakani mwa Kenya na Tanzania yenye urefu wa kilometa 100.2
Gharama
za upanuzi wa barabara ya Arusha - Tengeru na barabara ya kuzunguka nje
ya jiji la Arusha kwa upande wa Tanzania ni shilingi bilioni 209.6,
ambapo kati ya fedha hizo Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) itatoa
mkopo wa shilingi bilioni 190.2 na serikali ya Tanzania itatoa shilingi
Bilioni 19.4.
Aidha
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki ipo kwenye mazungumzo na serikali ya Japan ili kupata
mkopo wa ujenzi wa awamu ya pili inayoanzia Tengeru hadi Holili.
Kwa
upande wa Kenya, mradi huu unahusisha ujenzi wa barabara mpya kwa
sehemu ya Taveta hadi Mwatate yenye urefu wa kilometa 100. Sehemu ya
Mwatate hadi Voi ujenzi wake umekamilika.
Akizungumza
katika hafla hii, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambaye ni mwenyekiti wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki, amesema wananchi wa Afrika Mashari
hawapaswi kuwa masikini na kueleza kuwa mradi huo na mingine
itakayotekelezwa chini ya ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
itasaidia kuinua hali ya maisha ya wananchi.
Kwa
upande wao Marais Uhuru Muigai Kenyatta wa Kenya, Yoweri Kaguta
Museveni wa Uganda na wawakilishi wa marais wa Burundi, Rwanda, Sudani
Kusini wameuelezea mradi huo kuwa ni moja ya miradi muhimu ya kuimarisha
uchumi wa jumuiya ya Afrika Mashariki na wametoa wito kwa nchi zote
wanachama wa jumuiya hiyo kushirikiana kukuza biashara baina yake.
Viongozi
hao wote wamekiri kuwa Jumuiya hii yenye watu zaidi ya milioni 160,
inayo nafasi ya kupiga hatua kubwa za kiuchumi na kuondokana na
umasikini, ikiwa italitumia vizuri soko la pamoja kwa kubadilisha bidhaa
kutoka nchi moja hadi nyingine na kujenga viwanda vingi badala ya
kuendelea kutegemea bidhaa kutoka nje.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha
03 Machi, 2016
Post a Comment