BREAKING NEWS

Wednesday, 2 March 2016

Papa Francisko aliwasha moto wa matumaini!


 
Askofu mkuu Dieudonnè Nzapalainga wa Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati anasema, hali ya amani na utulivu wakati na baada ya mchakato wa uchaguzi mkuu na hatimaye Bwana Faustin-Archange Touadèra kutangazwa kuwa mshindi wa kiti cha Urais ni matunda ya imani na matumaini ambayo Baba Mtakatifu Francisko aliijengea Familia ya Mungu nchini humo wakati wa hija yake ya kitume Barani Afrika na mwanzo wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Leo hii familia ya Mungu nchini Afrika ya Kati imeanza kuona cheche za mwanga wa amani na utulivu. Haya ni mawazo ambayo pia yameoneshwa na watu pamoja na taasisi mbali mbali ndani na nje ya Afrika ya Kati.
Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo iliwasaidia kuhisi upepo wa mabadiliko ambayo yamejikita katika misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya wananchi wa Afrika ya Kati kwa kukazia mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kukataa misimamo mikali ya kidini na kiimani; kwa kuambata amani na utulivu, kwani wote ni ndugu wamoja, licha ya tofauti zao za kidini na kiimani, mambo ambayo yanapaswa kuwa ni amana na utajiri mkubwa kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wa Afrika ya Kati katika ujumla wake.
Vita na machafuko ya kisiasa nchini Afrika ya Kati, yalipachikwa kuwa ni vita ya kidini kati ya Waislam na Wakristo, lakini wakasahau kwamba, nyuma yake, kulikuwepo wanasiasa waliokuwa wanataka kujijenga kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia. Baba Mtakatifu Francisko, tangu mwanzo alionesha kuwa ni shuhuda wa haki, amani na upatanisho na mjumbe wa huruma ya Mungu aliyetaka familia ya Mungu nchini humo kujipatanisha tayari kuvuka ng’ambo ya pili ya mto huku wakiwa wameshikamana kama ndugu wamoja ili kuchuchumilia msamaha, upatanisho, haki na umoja wa kitaifa, mambo msingi yanayoendelea kuvaliwa njuga kwa wakati huu.
Viongozi wa dini wamekuwa na mchango mkubwa katika kuhamasisha mchakato wa upatanisho, haki na amani nchini Afrika ya Kati. Baba Mtakatifu Francisko akaonesha kwamba, inawezekana waamini wa dini mbali mbali kutembeleana na kushikamana kwa dhati kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rais Touadèra amechaguliwa na wengi kama shuhuda wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Kwa sasa anakabiliwa na changamoto ya ujenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa.
Wakati huo huo, Askofu Juan Josè Aguirre Munoz  wa Jimbo Katoliki Bangassou anasema, wananchi wengi wanafurahia kwa sasa uwepo wa amani na utulivu, lakini Kikundi cha Waasi kutoka Uganda  LRA, kinachoongozwa na Bwana Joseph Kony bado kinaendelea kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu.

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree