Walimu wanane wa Shule ya Sekondari Mihama, Kata ya Kitangili, Wilaya ya
Ilemela Mkoani Mwanza, wamesimamishwa kazi, watano kati yao
wakishikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufanya mapenzi na wanafunzi.
Pia,
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo aliyetembelea shule hiyo jana,
amevunja bodi ya shule hiyo baada ya kubainika kutofanya kikao hata
kimoja tangu ilipoteuliwa Aprili 24, 2013.
Pamoja na Mkuu wa
Shule, Joseph Malifedha, walimu wengine waliotiwa mbaroni jana ni
Rodrick Uroki, Denis Sanga, Edmund Boaz, Steven Samuel.
Walimu
watatu waliokuwa wakifundisha shuleni hapo, lakini wakahamishwa na hivi
sasa wanasakwa na polisi kwa tuhuma hizo ni Joseph Lamongi na Joeza
Mzava waliohamia Sekondari ya Sangabuye pamoja na Abdallah Mtelwe
aliyehamia Tanga.
Malifedha anadaiwa kuwachangisha fedha
wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha tatu kwa ajili ya picha za kuweka
kwenye vitambulisho (passport size).
Akitangaza uamuzi huo,
Mulongo alisema tume maalumu ya uchunguzi iliyoundwa Januari 27,
kuchunguza tuhuma dhidi ya walimu hao kujihusisha na mapenzi na
wanafunzi imebaini ukweli baada ya kuwahoji wanafunzi kadhaa.
“Ni
fedheha na haivumiliki kuona walimu wakifanya mapenzi na wanafunzi wao.
OCD wakamate walimu wote na uanze uchunguzi mara moja na kukusanya
ushahidi utakaowezesha wahusika kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue
mkondo wake,” aliagiza Mulongo.
Amri hiyo ilitekelezwa mara moja kwa walimu hao kuwekwa chini ya ulinzi.
Mulongo
pia alimwagiza Katibu wa Idara ya Utumishi wa Walimu Mkoa wa Mwanza,
Genzi Sahani kuwaandikia barua za onyo walimu wa kike shuleni hapo kwa
kushindwa kulinda na kutetea masilahi ya wanafunzi wa kike waliokuwa
wakidhulumiwa kingono na walimu wenzao kiasi cha baadhi yao kuathirika
kisaikolojia.
Pia, alimwagiza Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza,
Khamisi Maulid kuangalia uwezekano wa kuwahamishia shule nyingine
wanafunzi waliodhulumiwa kingono na walimu wao ili kuwaepusha na
matatizo ya kisaikolojia.
Maulidi alisema wanafunzi walioathirika zaidi ni wale wa kidato cha nne.
Katibu
wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Mkoa wa Mwanza, Said Mselem alisema
kitendo hicho kimeifedhehesha taaluma ya ualimu na kuahidi kuwa ofisi
yake itatanua wigo wa uchunguzi hadi kwenye shule nyingine.
Post a Comment