Saturday, 12 March 2016
Lengo ni wokovu wa roho za watu!
Posted by Unknown on 20:31:00 in | Comments : 0
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 12 Machi 2016 amewashukuru na kuwapongeza viongozi wa Mahakama kuu ya Rufaa ya Vatican, Rota, Romana kwa kuendelea kuwekeza katika majiundo makini katika huduma za kichungaji mintarafu mchakato wa masuala ya ndoa “Super rato”, yaani Ndoa imefungwa na tendo la ndoa kufanyika! Baba Mtakatifu katika hotuba yake anafafanua kwamba, wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia, Mababa wa Sinodi walionesha kiu ya kutaka kuona mchakato wa kutengua ndoa tete unafanyika haraka na kwa umakini mkubwa, kwani wanandoa wakati mwingine wanateseka sana kutokana na kutokuwa na uhakika wa hali ya maisha ya ndoa yao kiasi kwamba, hata Sakramenti ya Ndoa inakuwa mashakani!
Baadhi ya waamini wanashindwa kufikisha mawazo yao kwa vyombo vya Kanisa vinavyohusika na mchakato huu kutokana na urasimu na matokeo yake, Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia wakataka mchakato huu kurahisishwa zaidi. Kanisa kwa kusukumwa na upendo pamoja na huruma, limeamua kusikiliza kilio cha watoto wake wanaotaka haki itendeke kwa kujibu kilio hiki na Waraka wa “Mitis Iudex Domini Iesus na Mitis et Misericors Iesus” Yaani: Yesu Hakimu mwenye huruma na Haki na Huruma ya Yesu. Tume maalum iliyoundwa kunako mwaka 2014 ikafanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja na hatimaye kutoa matunda yake kwa ajili ya waamini.
Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema lengo la Nyaraka hizi ni shughuli za kichungaji zinaonesha utayari wa Mama Kanisa kwa wanandoa wanaosubiri kuhakikisha hali ya maisha ya Sakramenti yao ya Ndoa. Hapa hukumu mbili zimefutwa na matokeo yake hukumu fupi imepitishwa kwa kurejesha tena nafasi ya Askofu mahalia kama Hakimu wa kesi hii na kwa njia hii, nafasi ya Askofu imepewa mkazo wa pekee katika masuala ya Ndoa. Kisheria sasa Askofu anakuwa na dhamana ya kutoa maamuzi kuhusu uhalali wa Sakramenti ya Ndoa.
Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba sheria hizi mpya zinafahamika na kutafakariwa kwa kina, katika umuhimu na moyo wake, hususan miongoni mwa wafanyakazi wa Mahakama za Kikanisa, ili kuweza kutoa huduma ya haki na upendo kwa familia. Kwa watu ambao wameishi katika hali ya maisha ya ndoa tenge, uhakiki wa hali ya maisha yao ya ndoa unakuwa ni nafasi nyingine tena kuanza mchakato mpya wa maisha, daima ikiwa ni kwa ajili ya wokovu wa roho za waamini sheria kuu ndani ya Kanisa!
Hili ndilo himizo linalotolewa kwa wale wote ambao wameshiriki katika kozi hii ambayo imeandaliwa na Mahakama kuuu ya Rufaa ya Vatican, Rota Romana. Kanisa ni mama na mwalimu linapenda kuonesha uso mwaminifu wa Mungu na upendo wenye huruma wenye uwezo wa kumrejeshea mwamini nguvu na matumaini. Waamini waweze kuwa na ujasiri wa kuanza ukurasa mpya wa mahusiano yao, huku wakishiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Jumuiya ya Kanisa. Huu ni mchakato wa kuwahudumiwa waamini waliojeruhiwa wanaotaka kuhakikishiwa ukweli wa maisha na hali yao ya Ndoa; Kanisa pia linawaangalia kwa moyo mkuu wale wote wanaoendelea kuvumilia na kuwa waaminifu katika kifungu cha Sakramenti ya Ndoa, licha ya magumu na changamoto nyingi wanazokumbana nazo katika maisha yao. Mashuhuda waaminifu wa Sakramenti ya Ndoa wanapaswa kupongezwa na kuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa.
Kuna waamini wanaojitisha Misalaba mizito anasema Baba Mtakatifu katika maisha yao, ili kulinda na kudumisha misingi ya ndoa; ni waaminifu wakati wakiwa na afya na pale magonjwa yanapowaandama; wakati wa shida na mahangaiko ya ndani, daima uaminifu umekuwa ni dira na mwongozo wao wa maisha ya Ndoa! Baba Mtakatifu anawatakia mema katika huduma yao ya kuhakikisha kwamba, haki inatendeka, mwaliko wa kuishi utume huu kama huduma kwa waamini wenye madonda makubwa mioyoni mwao!
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment