BREAKING NEWS

Tuesday, 1 March 2016

January Makamba Aikosoa Serikali ya Kikwete



 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba ametofautisha nyakati za utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne iliyoongozwa na Dk. Jakaya Kikwete na zilizopita na huu wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, huku akiitoa kasoro iliyopita.

Makamba ameeleza kuwa wakati tawala zilizopita, watu walikuwa wakionewa haya na na kujuana kulichukua nafasi tofauti na awamu hii inayochukua hatua stahiki bila kujali.

“Nadhani moja ya changamoto zilizosababisha huko nyuma tusifanikiwe sana katika suala la uwajibikaji, ni hili suala la kuoneana haya. Suala la kujuana kidogo na kusitiriana,” Makamba aliliambia Gazeti la Mwananchi hivi karibuni.

Alisema kuwa utamaduni huo unapoendelea na kuota mizizi, suala la uwajibikaji huwa kikwazo na hatua stahiki dhidi ya watu wanaofanya makosa hushindwa kuchukuliwa.

Makamba ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia katika Serikali ya Awamu ya Nne, alieleza kuwa hatua za utumbuaji majipu zinazochukuliwa hivi sasa dhidi ya wakwepa kodi na watumishi wanaovunja sheria na kutowajibika ni sahihi na kwamba kama kuna mtu anaona anaonewa bado anayo nafasi ya kutafuta haki yake kwenye vyombo vya kisheria.

“Kikubwa tu ambacho mimi ninaamini ni kwamba kunahitajika kujenga utamaduni mpya wa watu kuogopa na kuheshimu wajibu wao, na kwamba hizi kazi si kazi zetu za kudumu. Wakati wote unapofanya makosa basi kuna Mamlaka ya kukuchukulia hatua,” alisema.

Makamba alisisitiza kuwa ni sahihi kuchukua hatua hivi sasa dhidi ya makosa yaliyofanyika katika utawala uliopita, “Kama huko nyuma hakukuwa na utashi wa mfumo wa kuwezesha makosa hayo kubainika, lakini utashi huo upo sasa, basi hatua zichukuliwe.”

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree