Monday, 7 March 2016
Imarisheni imani, matumaini na mapendo!
Posted by Unknown on 15:04:00 in | Comments : 0
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi, tarehe 5 Machi 2016 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kutabaruku Altare ya Kanisa kuu la Bikira Maria wa Bruna Jimbo Katoliki la Matera, Italia, baada ya kuhitimisha kazi kubwa ya ukarabati iliyodumu kwa kipindi cha miaka kumi na mitatu. Hii imekuwa ni fursa pia ya kufungua Lango la Huruma ya Mungu kama sehemu ya uzinduzi rasmi wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu Jimbo Katoliki la Matera. Ibada hii imehudhuriwa na umati mkubwa wa Familia ya Mungu Jimboni humo.
Katika mahubiri yake, amewapatia waamini wa Jimbo Katoliki Matera salam na matashi mema kutoka kwa baba Mtakatifu Francisko. Amekazia umuhimu wa Kanisa kuu kama kiini cha maisha ya Liturujia, mahali ambapo Askofu anatekeleza wajibu wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ni mahali panaposhuhudia umoja wa Kanisa na udugu kati ya waamini; mahali ambapo ubinadamu unakutana na utukufu wa Mungu. Hapa waamini wanapata nafasi ya kusikiliza Neno la Mungu, kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa, tayari kutubu na kumwongokea Mungu; kwa kuonesha upendo wa dhati kwa Mwenyezi Mungu pamoja na jirani.
Kanisa kuu ni kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake na kwa namna ya pekee, wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, tayari kukimbilia na kuambata huruma, upendo na msamaha wa Mungu, unaopaswa pia kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Lango la Huruma ya Mungu ni kielelezo cha huruma ya Baba wa mbinguni, mwaliko wa kuanza hija ya kuondokana na chachu na madhara ya dhambi, ili kupokea na kuambata furaha ya huruma na msamaha unaobubujika kutoka kwa Mungu.
Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni kipindi cha kukua na kukomaa katika imani inayoshuhudiwa katika matendo, kielelezo makini cha imani tendaji. Ni muda muafaka wa kuimarisha matumaini, huruma na msamaha. Waamini wawe tayari kumachia Kristo nafasi ili aweze kuyapyaisha maisha yao ya kiroho mintarafu mwanga wa Injili. Waamini wajitahidi kufanya ukarabati wa mioyo yao, kwa kumfungulia Kristo malango ya maisha yao, ili awabariki, awasamehe na kuwalinda. Awapatia mwanga wa Roho wake Mtakatifu ili aweze kuziangazia akili na nyoyo zao, ili waweze kuwa ni watu wema na watakatifu!
Pale waamini wanapotambua kwamba, wamekwenda mbali na uwepo wa Baba mwenye huruma kama ilivyokuwa kwa mwana mpotevu, wapige moyo konde, waanze mchakato wa toba na wongofu wa ndani, tayari kurudi na kumuungamia Mungu dhambi zao; Mungu ambaye yuko tayari kuwapokea na kuwasamehe dhambi zao. Ikumbukwe kwamba, furaha ya kweli inapatikana kwa kujenga umoja na udugu; kwa kuheshimu na kutekeleza Sheria za Mungu; kwa kuwajibika na kuwa na matumizi bora zaidi ya uhuru binafsi. Pale mwamini anapokufa kutokana na dhambi, awe na ujasiri wa kukimbilia na kuomba huruma ya Mungu. Hata kijana mkubwa anayesimulia na Mwinjili Luka katika mfano wa Baba mwenye huruma anapaswa pia kuonesha unyenyekevu na kushiriki furaha ya familia kama anavyoshuhudia Baba mwenye huruma. Huu ndio upendo unaovuka mipaka ya kibinadamu kwa kuwaambata wote.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment