BREAKING NEWS

Saturday, 5 March 2016

Furaha ya kweli ni matunda ya toba na wongofu wa ndani!




 Leo tunaadhimisha Dominika ya nne ya Kipindi cha Kwaresima katika Mwaka C wa Liturujia ya Kanisa. Kwa desturi Dominika hii inaitwa Dominika ya furaha. Ni Dominika inayotuingiza katika hali ya furaha kwa matendo makuu ambayo Mwenyezi Mungu anatutendea kwa sababu anaidhihirisha huruma yake kuu na ya milele. Antifona ya Zaburi ya mwanzo inatualika katika furaha hiyo: “Furahi, Yerusalemu, mshangilieni ninyi nyote mmpendao; furahini ninyi nyote mliao kwa ajili yake, mpate kunyonya, na kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake”. Mji wa Yerusalemu ulikuwa umeharibiwa sana na kuwaacha wakazi wake katika maombolezo lakini sasa kwa msaada wa Mungu unajengwa upya. Mji huo mpya unaoneshwa katika namna ya kuwa na kila aina ya baraka za Mungu; umejaa wingi wa vyakula na vinywaji tofauti na mji uliokuwa katika hali ya uharibifu. Kwa hakika hii ni habari ya furaha ambayo inafuta machozi na huzuni yote.

Katika Waraka wa Uso wa huruma kwa ajili Mwaka wa huruma ya Mungu tunaambiwa kwamba: “Mbele ya ukubwa wa dhambi, Mungu anajibu kwa msamaha kamili. Huruma itakuwa daima kubwa kuliko dhambi yoyote, na hakuna awezaye kuuwekea mipaka upendo wa Mungu anayesamehe daima”. Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba “Nitafurahi kufungua Mlango Mtakatifu katika sherehe hiyo ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili. Siku hiyo Mlango Mtakatifu utakuwa Mlango wa Huruma, ambao kwa njia yake yeyote aingiaye ataonja mapendo ya Mungu anayefariji, anayesamehe, na anayetupatia tumaini”. Huruma ya Mungu ndiyo sababu ya furaha kwetu kwani huruma hiyo inatufunulia upendo mkuu wa Mungu na kuufungua mlango wa matumaini.
Furaha tunayoipata katika Dominika ya leo inaanza kujionesha katika somo la kwanza. Inajionesha kwa Mwenyezi Mungu kuwarejesha tena wana wa Israeli katika nchi yao. “Siku hii ya leo nimeivingirisha hiyo aibu ya Misri iondoke juu yenu.” Sasa wanaweza kuvuna mazao waliyopanda katika nchi yao, wamekuwa watu huru. Sasa wametoka katika hali ya utumwa na safari ya kuifikia nchi hii ya ahadi imekamilika. Chakula kile cha safari walichopewa na Mungu kimekoma na wanakula mazao ya nchi. Kwa hakika wanaimba pamoja na mzaburi wakisema: “Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema”. Huu ni uthibitisho wa umilele wa upendo wa Mungu na uaminifu wake katika kutimiza ahadi zake. Pamoja na wingi wa dhambi zake Upendo wa Mungu unakuwa na nguvu zaidi na unanuia kumrejeshea tena mwanadamu hadhi yake aliyoipoteza kwa uasi.
Tunapofanya toba maana yake tunaamua kutengeneza na Mungu na tunapotengeneza na Mungu daima tunapata manufaa tele. “Wamtumainio Bwana ni kama mlima Sayuni, ambao hautatikisika, wakaa milele” (Zab 125:1). Mwana mpotevu ni mfano thabiti wa mmoja anayegundua kukengeuka kwake na kurudi katika mstari ulinyooka. Mwanzoni alijiona kwamba kukaa mbali na Baba yake atakuwa huru na kupata hadhi zaidi. Yeye alijidanganya katika kutafuta furaha kutoka katika mambo ya dunia hii. Matokeo yake ni kuingia katika udhalilishaji wa hali ya juu kiasi cha kutaka kujisawadhisha na nguruwe. Kwa mila na desturi za kiyahudi nguruwe ni mnyama mchafu na asiye na tamanika kwa namna yoyote. Lakini kijana huyu anapofikia hali hiyo inamaanisha kwamba alifikia udhalilishwaji wa hali ya juu kabisa.
Alipozingatia moyoni mwake aligundua kwamba mahali alipo si mahali pa kumpatia furaha ya kweli. Kwa Baba yake hata watumishi wanafuraha ya kweli. Neema ya Mungu inaingia ndani mwake naye anaitikia: “Nitaondoka, nitakwenda kwa Baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako”. Ni nafasi ya kujitafakari njia yetu na hamu yetu ya kutafuta furaha. Fedha nilizo nazo zinaweza kuonekana kunipatia furaha lakini furaha hiyo haikamiliki kama isipojengwa katika Mungu. Hali kadhalika mali zangu na hata madaraka yangu katika jamii. Inanisaidia nini kuwa na fedha hizo wakati nakosa kuonesha upendo kwa wenzangu walio wahitaji? Furaha yangu ipo wapi wakati bado ninazidi kuwafungia wenzangu vioo kila uchwapo? Je, wakati mwingine hatuamishii furaha zetu kwa viumbe ambao tunatamani kuwapa hadhi ya kibinadamu pasipo mafanikio?
Mtume Paulo alituonya Dominika iliyopita kwamba: anayedhania kwamba amesimama na aangalie asianguke”. Ili nalo linatugusa leo hii na hasa tukimtafakari kijana aliyebaki nyumbani kwa Baba yake. Pengine waweza kujipumbaza kuwa unamtii Baba yako kwa kufuata taratibu zote za nyumbani lakini katika hali ya utumwa.Hali hii haiwezi kukupatia furaha kwani mara nyingi unaingia katika huzuni, malalamiko na kujiona unaonewa. Hii umpata mwanadamu pale anapotenda si kwa ajili ya kuhudumia wenzake, si kwa ajili ya huduma yake kadiri ya kipawa alichopewa bali kutenda kwa ajili ya kupokea tuzo. Furaha yake inapatikana katika tuzo atakayoipata na si ufanisi katika kazi yake. Tunasahau kwamba kuwa ndani ya familia ya Mungu, yaani kuwa na upendo kwa Mungu na kwa wenzako ndiyo tuzo kubwa tunayopaswa kuitafuta katika maisha yetu. Je, katika jamii yetu hawapo wale ambao wanachuchumilia kutumikia lakini ni kwa ajili ya kuchuma tu na si ufanisi wa kazi yao? Tunashuhudia mengi kutoka kwa wengi ambao huduma zao hazidumu sababu tu wanasaka mahali penye maslahi.
Tunapokuwa ndani ya Kristo, asemavyo mtume Paulo katika somo la pili tunakuwa viumbe vipya, “ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya. Safari yetu ya toba katika kipindi hiki cha Kwaresima inalenga kutufikisha katika upya huu wa maisha, hali ambayo inatufanya kutengeneza na Mungu na kuwa katika furaha ya kweli. Kristo anakuwa mshenga wetu. “Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye”. Ni mwendelezo wa tendo la Mungu la kuutengeneza upya ubinadamu wetu kama tulivyoalikwa mwanzoni. Huu ni upendo wake kwetu usio na kipimo ambao daima unawaka ndani mwake na kumsukuma kumtafuta mwanadamu aliyepotea apate kurudi. Kwa nini hali hii isitupatie furaha?
Mwaka huu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni wakati maalum wa kuitambua neema hiyo ya Mungu. Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu unanuia kutupeleka katika furaha ya kuwa waana wa Mungu. Ni wakati  wa kuendelea kuionja neema hii ya Mungu inayofunuliwa kwetu, ni wakati wa kuishi katika hali ya matumaini kwa sababu ya upendo mkubwa wa Mungu kwetu. Basi, ninakualika leo kuijongea furaha ya Bwana na kukaa ndani mwake kwa kufurahia matunda ya neema zake anazotumwagia kila uchwapo.

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree