Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene amesema
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, imetumia busara kuahirisha
uchaguzi wa Meya uliopangwa kufanyika leo.
Juzi halmashauri
hiyo, iliahirisha uchaguzi huo, ikiwa ni mara ya pili baada ya kubaini
nyongeza ya wajumbe 14 katika orodha iliyowasilishwa kwa wakurugenzi wa
Manispaa za Kinondoni na Ilala.
Kasoro hizo zilijitokeza katika
kikao cha viongozi wa halmashauri hiyo kilichongozwa na Kaimu Mkurugenzi
wa Jiji, Sarah Yohana na kuhudhuriwa na viongozi wa CCM, Chadema na CUF
kujadili ajenda mbili.
Ajenda hizo ni taratibu za kuendesha uchaguzi wa Meya na kupitia orodha ya wajumbe wanaostahili kushiriki.
Kutokana
na hali hiyo, ilimlazimu Yohana kuwaagiza wakurugenzi wa manispaa za
Kinondoni na Ilala kuyafanyia uhakiki majina hayo wakishirikiana na
viongozi wa vyama ili kuyapeleka halmashauri kesho kutwa.
Simbachawene
alisema jana kuwa halmashauri na viongozi wa vyama hivyo walitafakari
maelezo aliyoyatoa awali kabla kufikia hatua ya uchaguzi huo.
“Sijapata
taarifa za kuahirishwa ndiyo kwanza nasikia kwako, lakini kama sababu
ndiyo uliyoniambia basi wamefanya jambo jema. Kwa sababu uchaguzi huu
una mvutano hivyo ni lazima mambo yaende kwa makubaliano.
“Pia
ni hatua nzuri, itakayoleta maelewano baina yao ili kupata haki sawa kwa
wajumbe watakaostahili kupiga kura. Tamisemi kazi yetu ni kueleza
sheria inasemaje,” Simbachawene.
Hivi karibuni, Simbachawene
aliahirisha uchaguzi huo, kisha kutoa sababu kuwa ni kuandaa mfumo wa
upatikanaji wa wajumbe kutoka manispaa tatu kwa kuwa ule wa chama kimoja
haukuwa na shida kama ilivyo sasa.
Katibu wa Chadema, Kanda ya
Dar es Salaam, Henry Kilewo alisema kukwama kwa uchaguzi huo kunatokana
na viongozi kutosikiliza mawazo ya upinzani.
“Januari 27, nilimwandikia
barua Simbachawene ya kutaka atupatie utaratibu wa uchaguzi huu
utakavyokuwa, lakini hadi leo (jana), hakunijibu ndiyo maana matatizo
kama haya yanatokea,” alisema.
Post a Comment