Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia
salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali
Ernest Mangu kufuatia vifo vya askari watatu waliopoteza maisha katika
ajali ya gari iliyotokea jana tarehe 06 Februari, 2016 katika kijiji cha
Isuna, Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida.
Askari waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni Inspekta Miraji Mwegelo, Sajenti Elias Mrope na Sajenti Gerald Ntondo.
Katika
salamu hizo Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa na vifo vya askari
hao, ambao wamekutwa na mauti wakiwa wanatekeleza majukumu yao ya
kikazi.
"Kupitia
kwako Mkuu wa Jeshi la Polisi natoa pole nyingi kwa familia za Askari
waliopoteza maisha, Ndugu, Jamaa na Marafiki pamoja na askari wote wa
Jeshi la Polisi Tanzania ambao wameguswa kwa namna ya pekee na msiba
huu" Amesema Rais Magufuli.
Ameongeza
kuwa anaungana na wote walioguswa na vifo hivyo katika kipindi hiki
kigumu, na amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi,
Amina.
Rais
Magufuli pia amewatumia salamu za pole Askari walioumia katika ajali
hiyo, akiwemo Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani katika Mkoa wa
Singida Mrakibu wa Polisi Peter Magira na kuwaombea wapone haraka ili
waweze kuendelea na majukumu yao ya kila siku.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
07 Februari, 2016
Post a Comment