Maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukeketaji Duniani: TGNP yaunga mkono Wanaharakati Kipunguni Dar es salaam
Kama sehemu ya kuadhimisha Siku ya Kupinga Ukeketaji Duniani, TGNP Mtandao kwa ushirikiano na Shirika la Watu Duniani (UNFPA), wanaharakati, Jamii ya Kipunguni, Dar es salaam imefanya majadiliano yaliyowashirikisha wananchi wa eneo hilo, viongozi wa serikali za mitaa, viongozi wa dini na vyama vya siasa pamoja na waandishi wa habari lengo likiwa ni kuweka mikakati ya kupambana na ukeketaji.
Katika ufunguzi, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao Bi. Grace Kisetu ameeleza kuwa lengo la kuadhimisha siku hiyo ni kuileta jamii pamoja katika kujadili hali ilivyo, kutambua changamoto na kutafuta njia nzuri za kukabilina na tatizo la ukeketaji.
“Takwimu za mwaka 2010 zinaonesha kuwa, takribani asilimia 15 ya wanawake Tanzania wamekeketaji hivyo mnaweza kuona bado tuna kazi kubwa kwani vitendo hivyo vinaendelea” Ameeongeza Bi. Kisetu
Aidha ameeleza kuwa pamoja na Tanzania kuridhia mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa inayomlinda mwanamke pamoja na kutunga Sheria Namba 16 ya Kanuni za Adhabu ambayo inatoa adhabu ya kifungo cha miaka mitatu hadi kumi na tano, bado vitendo vya ukeketaji vinaendelea nchini.
Alitaja mikoa inayoongoza katika ukeketaji ikiwa ni pamoja na Manyara,(71%), Dodoma, (64%), Arusha, (59%), Singida,(51%) Mara (40%), Morogoro, (21%) na Tanga ( 20%).
Akiwasilisha shughuli zinazofanywa na Kikundi cha Sauti ya Wananchi Kipunguni katika kupambana na ukeketaji katika kata hiyo, Mwenyekiti wa kikundi hicho Seleman Bishagazi amesema, kitendo hicho kimekuwa kikifanyika kwa siri kubwa. Amesisitiza kuwa baadhi ya familia za makabila yanayofanya ukeketaji katika eneo hilo huwafanyia ukeketaji watoto wao punde tu wanapozaliwa hivyo kuongeza changamoto zaidi.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kipunguni Mohamed Msofe ameahidi kutafuta ofisi kwaajili ya kikundi hicho ili kiweze kufanya shughuli za harakati kwa ufanisi zaidi hasa katika kuleta maendeleo.
”Nawaomba viongozi wa dini, waalimu na wanaharakati kuendelea kushirikiana katika kutoa elimu na nawahimiza Sauti ya Wananchi Kipunguni kutoa elimu kuhusu ukeketaji kwa njia ya sanaa katika mikutano ya wananchi”
Mkuu wa Dawati la Jinsia kutoka kituo cha polisi Lydia Mrema amewataka wananchi kushirikiana na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa na ushahidi ili haki iweze kutendeka. ”ushahidi ndio unaomtia mtu hatiani, lakini changamoto ni kuwa ushahidi unakuwa hafifu kwani wahusika huwa wanafamilia” Alisisitiza Lydia
Akitoa neno la kufunga mjadala huo, Mwakilishi wa UNFPA nchini Mary Nsemwa emesema kuwa wanawake kati ya milioni 100-140 wamekeketwa duniani huku ukatili huo ukifanyika katika nchi 28. Alieleza kuwa ukeketaji ni ukiukwaji wa haki za binadamu na kusisitiza kuwa pamoja na utoaji wa elimu, watu wanaohusika lazima wafikishwe kwenye vyombo husika.
“tunawapongeza kwa kazi nzuri na tutaendelea kuunga mkono juhudi za kupambana na ukeketaji”. Alisisitiza Mary
Mwakilishi mwingine wa UNFPA Tausi Hassan alisema “kuna hatari ya kuongezeka kwa idadi ya matukio ya ukeketaji kwani katika utafiti uliofanywa mwaka 2010 Dar es Salaamu ilikuwa na wastani wa asilimia 0.3 lakini utafti huu ukifanyika idadi itaongezeka”.Hii ni kwa sababu wenyeji wanaotoka mikoa inayofanya mila ya ukeketaji wamehamia na kuishai hapa”.
Tukio hilo linakuja siku mbili kabla ya siku rasmi ya maadhimisho hayo ambayo hufanyika tarehe 6 Februari kila mwaka. Siku hiyo inayoratibiwa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, huwaleta pamoja wadau katika kujadili masuala ya kisera, kisheria na kiutendaji katika kukabiliana na ukeketaji.
Post a Comment