HOSPITALI
ya Taifa ya Muhimbili (MNH) iliyopo jijini Dar es Salaam imesema ndani
ya siku 100 za kuwepo madarakani kwa Rais John Magufuli, imefanikiwa
kuongeza mapato kwa kiwango cha asilimia 90.
Pia,
imeongeza huduma za upasuaji wa dharura na pia kufanikisha upatikanaji
wa dawa kwa asilimia 96. Aidha, hivi karibuni inatarajia kuanzisha
chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU), kitakachokuwa
na uwezo wa kulaza wagonjwa 16 kwa wakati mmoja na kuwa na vitanda
kutoka nane hadi 25.
Hayo
yalisemwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Profesa
Lawrence Mseru wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam
jana.
Alikuwa
akieleza mafanikio ya hospitali hiyo katika siku 100 za kuwepo
madarakani kwa Dk Magufuli. Dk Magufuli aliingia madarakani rasmi
Novemba 5, mwaka jana baada ya kuapishwa kuongoza Serikali ya Awamu ya
Tano, akipokea kijiti cha kuiongoza Tanzania kutoka kwa Rais mstaafu
Jakaya Kikwete.
Akizungumzia
mafanikio hayo, Profesa Mseru alisema baada ya kuongezeka kwa kasi ya
usimamizi wa wafanyakazi na kupunguza kero za wafanyakazi, MNH imeongeza
uzalishaji wenye tija kwani kwa Desemba mwaka jana ilizalisha mapato ya
Sh bilioni 3.3 kutoka wastani wa Sh bilioni 2.7 zilizozalishwa kwa
kipindi cha miezi mitano kuanzia Julai mwaka jana.
Aidha,
alisema kwa Desemba mwaka jana pekee, MNH ilizalisha mapato ya Sh
bilioni 3.3 na Januari mwaka huu ilizalisha Sh bilioni 4.3, ambazo ni
sawa na ongezeko la asilimia 60.
Lengo ni kufikisha Sh bilioni sita Julai mwaka huu. “Haya
ni mafanikio makubwa sana kwa upande wa mapato kuwahi kupatikana katika
kipindi kifupi cha miezi miwili tu. Tumeona hospitali ina fursa kiasi
gani ya kuzalisha kiasi kingi cha fedha na hivyo kujitosheleza kwa
kiwango kikubwa kuendesha shughuli zake,” alisisitiza Dk Mseru.
Profesa
Mseru alisema baada ya agizo la Rais Magufuli la kuitaka Bohari Kuu ya
Dawa Tanzania (MSD), kujenga duka la dawa katika hospitali hiyo, kwa
sasa MNH imefanikisha wagonjwa kupata dawa kwa zaidi ya asilimia 96
kutoka kwenye duka hilo na maduka ya dawa ya hospitali hiyo.
Alisema
wamefanikiwa kuboresha mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(Tehama) katika utoaji na uagizaji dawa, na wagonjwa wanaokosa dawa
katika maduka hayo, hospitali hiyo huzitafuta na kuzinunua dawa hizo kwa
ajili ya wagonjwa hao.
Alisema
kutokana na hali hiyo, kwa sasa ukosefu wa dawa hospitalini hapo,
umepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na kuimarika pia kwa utendaji ndani
ya hospitali hiyo.
Akizungumzia
deni la hospitali hiyo, ambalo kwa sasa ni Sh bilioni 5.7 kwa wazabuni
na watu wanaopeleka bidhaa zao na huduma, Profesa Mseru alisema tayari
wameanzisha mkakati wa kupunguza deni.
“Tunaishukuru
Serikali kwa kutusaidia kulilipa deni lote tulilokuwa tunadaiwa na
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambalo ni shilingi bilioni 4.6,” alibainisha.
Akizungumzia
ongezeko la upasuaji wa dharura, Mkurugenzi huyo alisema hospitali hiyo
imeamua kuanzia sasa upasuaji wowote wa dharura, utakaofanyika kwa saa
24 kupitia Idara ya Magonjwa ya Dharura.
“Tayari tuna vyumba viwili vya kisasa vya kufanyia upasuaji huo, awali tulikuwa na chumba kimoja tu,” alieleza na kuongeza kuwa katika kuboresha huduma, pia wanatarajia kuongeza vyumba vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu.
Kuhusu
kuboresha maslahi ya wafanyakazi, alisema ndani ya kipindi cha miezi
miwili menejimenti ya hospitali hiyo, imelipa wafanyakazi malimbikizo ya
madai yao ambayo ni kiasi cha Sh milioni 600.
Alisema
hospitali hiyo imeanza kulipa madeni hayo, yanayotokana na fedha za
mwito maalumu (on call), malipo ya wauguzi ya usiku, malipo ya posho
mbalimbali hususani kwa madaktari na kada nyingine za afya
zinazoshughulika na wagonjwa na likizo.
“Tumeanza
kulipa fedha hizi tangu Desemba na hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu
tunatarajia kumaliza deni hili lote. Kutokana na hatua yetu hii kwa sasa
morali ya wafanyakazi imeongezeka, jambo lililosaidia kuongeza mapato
ya hospitali,” alifafanua mkurugenzi huyo.
Aidha,
Profesa Mseru alizungumzia maagizo ya Rais Magufuli alipotembelea
ghafla hospitalini hapo Novemba mwaka jana na kusisitiza kuwa tayari
hospitali hiyo imetengeneza mashine zote mbili; MRI ambayo tayari
imeshapima wagonjwa 2,200 na CT Scan iliyopima wagonjwa zaidi 1,000.
Alisema
kutokana na mahitaji ya vipimo kupitia mashine za CT Scan, Serikali ya
Awamu ya Tano imeshanunua mashine mpya yenye uwezo wa slices 126, wakati
CT Scan ya awali ilikuwa na uwezo wa slices mbili tu na ina uwezo wa
kupima wagonjwa 50 ndani ya saa 24.
Kuhusu
agizo la kupunguza wagonjwa kulala chini, alisema hospitali hiyo
imejitahidi kupunguza tatizo hilo, ingawa imekuwa ngumu kutokana na
ongezeko kubwa la wagonjwa.
Alisema
hospitali hiyo ina mpango wa kupitia upya mfumo wa muundo wa kuona
wagonjwa wa nje, waliolazwa na wagonjwa wanaohitaji huduma za vipimo na
uchunguzi.
“Ndio
maana tunatarajia kuzindua Mkataba wa Huduma kwa Wateja, unaonesha
tumedhamiria kufanya nini na wateja watarajie nini kutoka kwetu,” alieleza.
Pia
alisema wana mpango wa kupunguza wagonjwa wanaokwenda nje kupata huduma
ya upandikizaji wa figo, kwani ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, MNH
itaweza kupandikiza figo nchini na kupanua huduma ya kusafisha figo
kutoka uwezo wa kuwa na mashine 23 hadi 50.
Novemba
5, mwaka jana, Dk Magufuli aliapishwa rasmi kuwa Rais wa Serikali ya
Awamu ya Tano. Siku nne baada ya kuapishwa kwake, alifanya ziara ya
ghafla Muhimbili ambako alivunja Bodi ya Wakurugenzi ya MNH na kumuondoa
madarakani Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Hussein Kidanto.
Dk
Magufuli alichukua hatua hiyo, baada ya kusikitishwa na taarifa ya
kutofanya kazi kwa mashine za CT- Scan na MRI kwa takribani miezi miwili
huku mashine kama hizo zikifanya kazi katika hospitali za watu binafsi.
Aidha,
kiongozi huyo alihuzunishwa na hali ya huduma kwa wagonjwa, hususan
wanaolala chini ikiwemo hali ya kutokujali wala kushughulikia vifaa vya
kufanyia kazi.
Post a Comment