BREAKING NEWS

Thursday, 25 February 2016

Serikali Yasema Bajeti Ijayo Itatekelezwa Kwa Fedha Za Ndani




SERIKALI imesema bajeti ya mwaka ujao, hususani utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo, itatekelezwa kwa fedha za ndani.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema miradi mikubwa kama vile ujenzi wa reli ya kisasa ya kati na miradi mingine mikubwa, ndiyo itajengwa kwa fedha za msaada kutoka nje kwa kuwa nchi haiwezi kukwepa kuomba msaada kutoka nje.

Alisema hayo jana katika mji mdogo wa Holili mpakani mwa Tanzania na Kenya, baada ya kuangalia shughuli za utendaji kazi katika mpaka huo na baadaye kuzungumza na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) katika mji huo.

Alisema makusanyo ya sasa ya Sh trilioni 1.7 kwa mwezi yanayokusanywa kwa sasa nchi nzima, fedha zake zitaelekezwa kwa shughuli za maendeleo kwa mikoa yote nchini. 
Waziri huyo alisema si kweli kwamba serikali ya Rais John Magufuli haitahitaji msaada wa fedha kutoka nje. “…la hasha! ila msaada huo hautakuwa mkubwa kama zamani,” alisema waziri.

Akizungumzia bajeti ijayo, alisema fedha zake nyingi zitatokana na makusanyo ya fedha za ndani na sio za msaada kutoka nje.

Waziri huyo alisema kwa asilimia kubwa bajeti ya miradi ya maendeleo katika mikoa yote nchini, fedha zake zitakuwa ni za ndani zilizokusanywa na kiasi kidogo cha fedha kitatoka nje.

Aliwataka watumishi wote wa umma, wanaokusanya mapato katika maduhuli ya serikali, kuacha mara moja kushika na kukusanya fedha kizamani kwa kutumia stakabadhi na kuandika kwa mkono ili kuepuka ushawishi wa kutumia fedha hizo kwa njia isiyokuwa halali.

Alisema anasikitishwa na utaratibu wa ofisa uhamiaji wa kitengo viza cha mji wa Holili, kukaa na fedha zaidi ya siku tano na kutoa stakabadhi kwa mkono.

Waziri alikemea na kumtaka ofisa wa uhamiaji wa mji wa Holili, kuacha mara moja kukaa na fedha za serikali kwa zaidi ya wiki, tofauti na mtunza fedha wa TRA anayepeleka fedha benki kila siku.

Alisema utaratibu huo ulishapigwa marufuku miaka mitatu iliyopita, lakini anasikitika unaendelea katika mji wa Holili. Alimwagiza Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, kubadilisha hali hiyo kwa maslahi ya serikali.

Akizungumzia uadilifu, Waziri Mpango aliwataka wafanyakazi wa TRA, kuacha kufanya kazi hiyo kwa kuwanyanyasa wafanyabiashara, kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria. Alisema uadilifu si wa mali tu, bali uko pia katika kutenda kazi za kila siku.

Alisema pia wananchi wanapaswa kulipa kodi kwa kufurahia na kuona kodi wanayolipa inawanufaisha, ikiwa ni pamoja na kufanya maendeleo katika miradi mbalimbali.

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree