Wajumbe wa Utume wa Sala wa Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina wanayo kila sababu ya kumshukuru mtakatifu huyu aliyewasaidia kugundua hazina ya maisha ya upendo wa Mungu kwa kuonja na kuguswa na msamaha na huruma ya Mungu. Padre Pio amekuwa ni mtumishi mwaminifu wa huruma ya Mungu, mtume aliyesikiliza kwa makini, akaganga na kuponya madonda ya dhambi katika maisha ya kiroho kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho na kusaidia kurejesha amani mioyoni mwao. Padre Pio alikuwa ni fundi mkubwa wa kuwapatia waamini harufu ya msamaha wa Mungu, uliokuwa unabubujika kutoka kwa Yesu Kristo mteswa, njia ya huruma ya Mungu.
Padre Pio alikuwa ni mtumishi mwaminifu wa msamaha na huruma ya Mungu
Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa wanachama wa Utume wa Sala wa Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina, Jumamosi tarehe 6 Februari 2016. Padre Pio alibahatika kuwapatia watu wengi waliokuwa wanateseka, upendo na huruma ya Mungu. Akafanikiwa kubeba ndani mwake Fumbo la mateso akawa kweli ni mfereji wa huruma ya Mungu uliolowanisha majangwa ya nyoyo za watu, akawajengea watu wengi chemchemi ya maisha mapya.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Padre Pio katika maisha na utume wake aliona kwamba, utume wa sala ulikuwa ni hazina ya imani na kielelezo cha upendo wa kimungu na wala si tu mahali ambapo kulikuwa kunatoa fursa kwa watu kukutana na marafiki pamoja na wajuani wao. Bali huu ni utume unaojikita katika maisha ya binadamu kwani sala inausukuma ulimwengu kusonga mbele sanjari na kuonesha kicheko cha baraka ya Mungu kwa mioyo na madhaifu ya watu.
Baba Mtakatifu anakaza kusema sala ni tendo la huruma kiroho linalotaka kuelekeza yote moyoni mwa Mwenyezi Mungu, kwa kujiaminisha kwa Mungu, Kanisa kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anaweza kutenda kadiri ya uradhi wake. Sala ni ufunguo wa moyo wa Mungu na nguvu kuu ambayo Kanisa limekirimiwa, ikiwa kama litaendelea kudumu katika umoja na kusali kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria. Baba Mtakatifu anaonya kwamba, ikiwa kama Kanisa litashindwa kusali vyema, matokeo yake litaegemea kwenye mambo ya juu juu kama vile fedha na mali; madaraka na matokeo yake mchakato wa Uinjilishaji unapotea na furaha kuzimika kama kibatari!
Baba Mtakatifu anawataka waamini kuhakikisha kwamba, utume wa sala unakuwa ni vituo vya matendo ya huruma, wazi na endelevu, ili kwa njia ya sala wanaweza kuona nguvu ya Mungu na upendo unaobubujika kutoka kwa Kanisa. Waamini wawe kweli ni mitume wa furaha ya sala changamoto kubwa iliyotolewa na Padre Pio kwa waamini wake. Kwa kuguswa na mahangaiko ya watu, akajenga Hospitali kubwa, ushuhuda wa matendo ya huruma kimwili, Hospitali iliyofunguliwa takribani miaka sitini iliyopita, hili ni Hekalu na Sala na Sayansi, mahali ambapo wagonjwa wanapata tiba muafaka sanjari na kuonjeshwa utu.
Hospitalini pawe ni mahali pa kupata tiba na kumhudumia mgonjwa; mahali pa kuganga mwili na kuponya magonjwa ya kiroho. Sala ina nguvu kubwa ya kuponya madonda ya ndani. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, hata wagonjwa waliokufani wanaweza kushiriki katika sala zinazoendeshwa na wale waliokaribu nao, kwa kujiaminisha kwa huruma ya Mungu.
Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wale wote wanaowahudumia wagonjwa kwa tija na ufanisi, kwa upendo na imani thabiti. Waamini wawe na ujasiri wa kuomba neema ya kutambua uwepo wa Kristo miongoni mwa wagonjwa na wale wote wanaoteseka, kama alivyokuwa anasema Padre Pio kwamba mgonjwa ni Yesu!
Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee, amewashukuru na kuwapongeza waamini wa Jimbo kuu la Manfredonia- Vieste-San Giovanni Rotondo, mahali ambapo Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa anakwenda mara nyingi ili kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kuungama pamoja na kuomba usahuri kutoka kwa Padre Pio ambaye alionekana kuwa ni sura hai ya Kristo mteseka na mfufuka. Kwenye uso wa Padre Pio kuna mng’ao wa mwanga wa ufufuko, changamoto kwa waamini pia kuwa na mng’ao wa mwanga wa mbinguni.
Post a Comment