Wakazi
wa Kitongoji cha Misungwi D, Kijiji cha Misungwi wilayani Misungwi,
Mkoa wa Mwanza wamemkataa Mwenyekiti wao, Raphael Kimoka (Chadema) kwa
tuhuma za kutowasomea taarifa za mapato na matumizi ya fedha tangu
achaguliwe.
Walitoa msimamo huo kwenye mkutano mkuu wa kitongoji uliofanyika juzi.
Ofisa
Mtendaji wa Kijiji cha Misungwi, Amos Seko alisema wakazi hao wamekuwa
wakishindwa kufanya shughuli za maendeleo, huku wakiendelea na vikao na
kuweka maazimio ya kutokuwa na imani na mwenyekiti wao.
“Leo
ni kikao cha mwisho kuhusiana na malalamiko yenu dhidi ya mwenyekiti
mliyoyaleta tangu Oktoba 27, mwaka jana. Mtaamua wenyewe hapa ama
aendelee au la,” alisema Seko.
Seko
alisoma tuhuma nyingine dhidi ya mwenyekiti zilizopelekwa kwake na
wakazi hao kuwa ni kutosimamia majukumu yake vizuri, kubagua wananchi
wakati wa kutoa huduma, kutohudhuria vikao vya kitongoji vya maafa na
kutetea uhalifu.
Mwakilishi
wa mkuu wa wilaya ambaye ni Ofisa Tarafa wa Misungwi, Peter Marco
alisema tuhuma dhidi ya mwenyekiti huyo ziliwasilishwa kwenye kikao cha
halmashauri ya kijiji cha Novemba 11, mwaka jana, Alisema kiongozi huyo
alipewa nafasi ya kujitetea, lakini hakufanya hivyo badala yake alitoka
nje ya kikao.
Kimoka
alipopewa nafasi ya kujitetea, alidai kuwa mkutano huo umeandaliwa
kisiasa, hivyo hautambui kwa sababu wengi wao ni wanachama wa CCM.
“Waliohudhuria hawakunitendea haki, sikubaliani nao,” alisema.
Aliongeza kuwa, kwa muda mrefu alijua kulikuwa na mpango wa kutaka kumuondoa madarakani wenye msukumo wa kisiasa.
Post a Comment