Mwenyekiti
wa Chama cha Mapinduzi Dkt Jakaya Mrisho Kikwete ametangaza rasmi
kuachia kiti hicho kabla ya mwezi Februari mwakani, huku akisema CCM
imesikitishwa na uamuzi wa ZEC kufuta uchaguzi wa Zanzibar.
Dkt
Kikwete ambaye pia ni Rais wa awamu ya nne wa serikali ya Jamhuri ya
Tanzania, ametoa tamko hilo leo katika sherehe za miaka 39 ya chama
hicho zilizofanyika katika uwanja wa Namfua mjini Singida, ambapo yeye
ndiye aliyekuwa mgeni Rasmi.
Katika
hotuba yake, Dkt Kikwete amewaeleza wana CCM waliofurika kiwanjani hapo
kuwa hizo ndizo zitakuwa sherehe zake za mwisho kwake kuhudhuria huku
akiwa mwenyekiti, kwa kuwa katika sherehe zijazo mwenyekiti wa chama
hicho atakuwa ni Rais John Magufuli.
"Hii
ni mara yangu ya mwisho kuhudhuria sherehe hizi kama mwenyekiti wenu,
Katika sherehe za mwakani, mwenyekiti wenu atakuwa ni Rais John
Magufuli"
Chama
hicho kinataraji kufanya maadhimisho yake ya miaka 40 ya kuzaliwa kwake
mwezi Februari mwaka 2017 mwaka ambao pia ni wa uchaguzi mkuu wa chama
hicho kwa mujibu wa katiba yao.
Kuhusu
Uchaguzi mkuu wa Zanzibar, Kikwete amesema wao kama CCM hawakupenda
uchaguzi huo urudiwe kwa kuwa walikuwa wana uhakika wa ushindi, na
tayari walikuwa wanajiandaa kusherehekea ushindi mnono, lakini
wanalazimika kukubaliana na maamuzi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa
kuwa hawana namna nyingine.
“Tulikuwa
tumejiandaa kushangilia, lakini Tume wakasema kuwa uchaguzi unafutwa
kwa kuwa kulikuwa na dosari kubwa, tukasikitika sana lakini kwa kuwa
tume wameamua, tukashauriana na wenzetu wa Zanzibar, tukaona ni bora
kukubali kurudia uchaguzi huo, lakini hatukupenda”
Amewataka
wana CCM wote visiwani Zanzibar kujiandaa na uchaguzi siku ya Machi 20,
mwaka huu na kwamba wahakikishe wanatunza shahada zao kwa ajili ya
kuchagua wagombea wa CCM.
Katika
hatua nyingine, Rais Kikwete ametumia nafasi hiyo kuelezea mafanikio ya
chama hicho katika kuwaletea watanzania maendeleo ambapo amesema katika
miaka yake 39, chama hicho kimefanikisha mengi ikiwa ni pamoja na
kuboresha miundombinu ya barabara.
Pia
amezungumzia mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ambapo licha ya
kukiri kuwa chama hicho kilikuwa kwenye wakati mgumu, amesema bado kiko
imara, na kitaendelea kuwa imara.
Amesema
licha ya baadhi ya watu kukitabiria kifo chama hicho, watanzania bado
wameendelea kukiamini na kukipa ushindi wa kishindo huku akitolea mfano
ushindi ambao chama hicho kimeupata katika ngazi ya urais, udiwani, na
ubunge mwaka 2015.
“Katika
ubunge sisi tumepata asilimia 73 ya viti vyote vya ubunge wa majimbo,
na hata katika udiwani tumeshinda asilimia zaidi ya 73 katika kata zote,
nashangaa kuna watu wanadai kwamba eti CCM haipendwi, yaani hata hesabu
zinawashinda..” Amesema Kikwete.
Akizungumzia
utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano, Dkt Kikwete amempongeza
Rais Magufuli kwa kufanya yale aliyotumwa katika Ilani ya CCM na kuahidi
kumpa ushirikiano ili ayafanikishe yote yaliyomo katika ilani hiyo.
Amewakosoa
watu wanaodai kuwa Magufuli hatekelezi Ilani ya CCM bali ya vyama
vingine na kusisitiza kuwa kila jambo linalofanywa na serikali hiyo limo
ndano ya ilani ya CCM.
Kikwete
ametolea mfano suala la kuanzishwa kwa mahakama maalum ya kushughulikia
rushwa na wahujumu uchumi na kusema kuwa suala hilo limo ndani ya ilani
ya CCM, na wala sio jambo la kuzuka.
Amesema wanaodai Magufuli anatekeleza sera zao wameishiwa na hawana la kuzungumza tena.
"Watani zetu wanasema anatekeleza mambo yao, wamekosa ya kusema wanasubiri akija bungeni watoke, watu wazima hovyooo"
Pia
amewataka wanachama wa CCM kuchagua viongozi bora na watakaoweza
kukijenga upya chama hicho katika uchaguzi wa chama hicho utakaofanyika
mwakani , huku akiwataka wajiandae kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka
2020.
“Mwisho wa uchaguzi mmoja ni mwanzo wa uchaguzi ujao, tumemaliza wa mwaka 2015 tuanze kujiandaa na uchaguzi wa 2020”
Post a Comment