BREAKING NEWS

Thursday, 4 February 2016

Mwanasheria Mkuu Akemea Wabunge Kushabikia Vurugu



Mwanasheria  Mkuu wa Serikali, George Masaju amewataka wabunge kusimamia utekelezaji wa sheria wanazotunga na si kuhamasisha uvunjaji wa sheria za nchi.
 
Alitoa kauli hiyo jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF).

Mbunge huyo alihoji kwa nini serikali haiwachukulii hatua watu wanaofanya uhalifu Zanzibar na kama wameshindwa, wananchi wawaadhibu wahalifu hao kwa kuwapiga mawe.
Pia Mbunge huyo alitaka Waziri wa Mambo ya Ndani atamke kama wameshindwa kudhibiti uhalifu huo, wananchi washughulikie wahalifu hao kwa kuwapiga mawe na magari yao.

Akijibu swali hilo mwanasheria mkuu wa serikali, alisema hoja ya Mbunge huyo sio sahihi na kusisitiza, “Waziri hawezi kutamka watu wavunje sheria, wabunge wanatunga sheria wanatakiwa kusimamia utekelezaji wake”.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angelah Kairuki alisema kuhusiana na hoja kuwa vyombo vya dola vinakiuka haki za binadamu, endapo mbunge huyo ana malalamiko awasilishe kwenye tume ya haki za binadamu ili yapate kushughulikiwa.

Mbunge wa Rombo, Joseph Selesini (Chadema) katika swali la nyongeza alihoji kwa kuwa matukio ya wananchi kuchukua sheria mkononi yanasababishwa na mambo mawili, ikiwemo polisi kwenda kwenye tukio wakiwa wamechelewa na wahalifu wanapokamatwa baada ya muda wanaachiwa.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni alisema Jeshi la polisi linajitahidi kufanya kazi, idadi ya polisi haitoshelezi kutokana na polisi mmoja kuhudumia watu 300 hadi 350.

“Wakati mwingine inatokea baadhi ya polisi wana mapungufu na wamekuwa wakichukuliwa hatua za kisheria na wale wanaotenda makosa ya jinai sheria imekuwa ikifuata mkondo wake,” alisema.

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree