BREAKING NEWS

Sunday, 28 February 2016

Mwachieni Mungu nafasi aandike upya kurasa za maisha yenu!




Ndugu wapendwa, karibuni tena katika dominika hii ya tatu ya kwaresima. Katika tafakari yetu dominika ya pili, tulialikwa kuyatambua mapenzi ya Mungu na utukufu wake. Tuliona jinsi Mungu anavyotimiza ahadi yake na jinsi anavyooneka katika sura yake halisi mbele ya wafuasi wake. Nasi tukaalikwa kuangalia sura ya imani yetu, ufuasi wetu na maisha yetu kama yanabeba sura ya kimungu. Huo ufahamu ambao unawekwa mbele yetu, leo hii twaalikwa kuuwajibikia au kuufanyia kazi. Na ndiyo wito wa neno la Mungu dominika hii ya leo.
Katika neno la Mungu dominika hii tunaona haja ya kukesha na kuongoka. Katika somo la kwanza leo, tunaona ufunuo wa Mungu kwa Musa na tangazo la mpango wa Mungu wa kuwakomboa Waisraeli toka utumwani. Mungu anajifunua kwa Musa, hata kutaja jina lake. Tukio hili linafanyika chini ya mlima Sinai, mahali walipoitwa Waisraeli. Musa anaishi maisha ya jangwani na Mungu anamtumia katika mazingira yake hayo kwa kazi ya baadaye. Katika sura hii ya tatu ya Kutoka tunaona ufunuo wa Mungu, tangazo la mpango wa ukombozi na wito wa Musa. Ujio huu unaonesha hali ya Mungu katika tendo la ukombozi. Musa lakini anapata wasiwasi – kazi hii ni ngumu ila bahati yake ni kuwa Mungu anajifunua
Katika somo la pili tunaona mtume Paulo anatumia mfano wa historia ya kutoka kuwaonya wakristo Wakorintho juu ya maisha yao ya kikristo. Mtume Paulo anasema haitoshi tu kusema naamini katika Kristo, hatuna budi kumfuata, kuwa wafuasi kweli.
Katika somo la injili tunaona mwito wa mwinjili Luka wa kubadilika. Sehemu hii ya maandiko matakatifu imeandikwa na mwinjili Luka tu. Tukio hili lilitokea wakati Wagalilaya walipokuja Yerusalemu kutoa sadaka na wakauawa na majeshi ya Pilato. Pia habari ya wale 18 waliouawa halipo katika injili nyingine isipokuwa katika Luka tu. Mnara wa Siloam ulikuwa katika kona ya kusini na mashariki ya mji. Ulivunjika wakati Pilato akiimarisha kuta ili kuongeza kiwango cha maji huko Yerusalemu.
 Inasemekana kuwa habari hii ilitajwa ili kumtaka Yesu awake hasira dhidi ya Pilato ili wapate sababu ya kumshitaki. Aidha Yesu anatumia nafai hii ili kuonesha haja ya kukesha na kuongoka. Na Yesu anathibitisha fundisho lake akitaja hali ya mtini usiozaa matunda n.k.
Hakika hatuna budi leo kukagua mpango wetu wa kwaresima na kuona kama unaendelea vizuri. Leo twaona tena Yesu akiongea habari ya jambo lililo kati yetu. Yohani alikuwa akiongea juu ya jambo lijalo. Na zaidi sana, tunakumbushwa kile tulichotamka siku tunaanza kipindi cha Kwaresima, tubuni na kuiamini injili – Mk.1:15. Huu ni mwaliko wa uzima, wa kutaka kuanza upya. Sote twajua kuwa ni vigumu kuacha mazaoea yetu lakini daima twaona jinsi anavyotuhimiza kufanya mabadilko ya ndani – Lk. 9:23 – kujikana nafsi na kuchukua msalaba, Lk. 16:16 – habari juu ya sheria ya Musa na sheria mpya ambayo hatuna budi kutumia nguvu kuingia ndani.
Tukumbuke kuwa hatuwi wakristo kwa hiari yetu bali ni neema ya Mungu inayofanya kazi. Hata maendeleo yetu ya ukristo wetu hayategemei nguvu zetu wenyewe. Ni upendo wa Mungu unaotujalia nguvu. Somo la kwanza laeleza wazi jambo hili. Twasikia habari juu ya Mungu aliye kati yetu. Uwepo unaofanya mageuzi na uongofu uwezekane kila siku. Sisi nafasi yetu ni kusikia sauti ya Mungu na kutimiza mapenzi yake.
Mtu mmoja alimwuliza Padre ni jinsi gani ajitolee maisha yake kwa Mungu, jinsi gani afanye ili apate kuongoka. Yule Padre alitoa karatasi nyeupe isiyoandikwa cho chote na kumwambia inatosha kuandika jina lako na kuweka saini chini/sehemu ya chini ya karatasi  na kumwacha Mungu ajaze mapenzi yake sehemu iliyobaki wazi. Nasi pia hatuna budi kumwachia Mungu aandike upya ukurasa wa maisha yetu. Hilo ndilo dai la maisha mapya ya kwaresima la kukesha na kuongoka.

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree