Friday, 12 February 2016
Moto Waua Askari Polisi Na Mpenzi Wake
Posted by Unknown on 05:18:00 in | Comments : 0
ASKARI wa kike wa Usalama Barabarani, Attuganile Mwakibete (37) na mpenzi wake Sunday Mhagama (36), wameteketea kwa moto baada ya nyumba walimokuwa ndani kuungua.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alisema tukio hilo lilitokea Februari 2, mwaka huu saa 7:15 mchana katika kitongoji cha Maporomoko, Kata na Tarafa ya Laela Wilaya ya Kipolisi ya Laela.
Inadaiwa kuwa nyumba hiyo iliyoteketea kwa moto ambayo askari Attuganile alikuwa amepanga vyumba viwili, ni mali Yaiyela Mwamahonje aliyokuwa akiishi na watoto wake wawili wadogo ambao wamenusurika kufa, licha ya kuwemo ndani ya nyumba hiyo wakati wa ajali hiyo.
Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa Mhagama aliyekuwa rafiki wa trafiki huyo wa kike, ni mkazi wa Mbeya ambako mkewe anaishi, na alikuwa na mazoea ya kumtembelea mpenzi wake huyo mara kwa mara.
Inadaiwa askari Attuganile alikuwa ameachana na mumewe wa ndoa. “Vyumba viwili yaani sebule na chumba walimokuwemo Attuganile na Mhagama viliwaka moto baada ya jenereta lililokuwa likifanya kazi likiwa sebuleni humo kulipuka na kuwajeruhi vibaya,” alieleza.
Kwa mujibu wa Kamanda Mwaruanda, Attuganile alifariki dunia Februari 8, mwaka huu saa 2:30 asubuhi akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga.
Mhagama alikimbizwa na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya jijini Mbeya ambako alifariki dunia Februari 9, mwaka huu. Kamanda Mwaruanda alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment