BREAKING NEWS

Monday, 22 February 2016

Ikimbileini huruma ya Mungu kwa toba na wongofu wa ndani!


Iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa Mwaka 2016. Katika ujumbe huu, Maaskofu wanachambua kwa kina na mapana huruma ya Mungu, ufunuo wa huruma ya Mungu kwa binadamu; Kanisa na huruma ya Mungu hapa kwa namna ya pekee Maaskofu wanakazia wajibu wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu, Umuhimu wa kupokea Sakramenti za Kanisa, Matendo ya huruma: kiroho na kimwili; Bikira Maria Mama mwenye huruma na mwisho wanahitimisha ujumbe huu kwa kuhimiza toba na wongofu wa ndani; upendo wa Kristo na wajibu wa waamini, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Baba wa mbinguni!
Fadhili za Bwana nitaziimba milele (Zab 89:1)
Wapendwa Mapadri, Watawa, Waamini Walei na watu wote wenye mapenzi mema: “Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana wetu Yesu Kristo”(1Kor 1:3). Tukiwa bado tunaendelea kuiishi tafakari ya zawadi ya maisha ya familia na maisha ya wakfu ya watawa, sisi Maaskofu wenu tunawandikieni barua yetu ya kusindikiza tafakari yetu ya mfungo wa Kwaresima. Tunaungana na Kanisa zima kutafakari juu ya fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, fumbo lililo kielelezo dhahiri cha huruma ya Mungu kwa wanadamu wote. Kama mjuavyo, tangu tarehe 08 Desemba 2015 Baba Mtakatifu Francisko alifungua rasmi Jubilei ya pekee ya Huruma ya Mungu itakayoendelea mpaka tarehe 20 Novemba 2016, siku ya Sherehe ya Bwana wetu Yesu Kristo Mfalme.
Tumependa tafakari ya Kwaresima ya mwaka huu iendane na wazo la Jubilee hii kwasababu huruma ni “daraja linalomuunganisha Mungu na mwanadamu,na kufungua mioyo yetu katika tumaini la kupendwa daima licha ya ukosefu wetu”. Kwa kuwa Mungu Baba yetu ametupenda na kututunza yatupasa sisi watoto wake kuhurumiana kama Baba yetu alivyo na huruma kwetu.
Katika sala ya ufunguzi ya Dominika ya ishirini na sita ya mwaka tunasali hivi: “Ee Mungu, wewe unaonyesha enzi yako kuu hasa kwa kusamehe na kutuhurumia”. Kuhurumia na kusamehe ni matendo ya Mungu ambaye ni mwenyezi. Na kimsingi Mungu ni huruma yenyewe. Katika Maandiko Matakatifu Mungu wetu anatambulika kuwa ni “Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli, mwenye kuwaonea huruma watu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe” (Kut 34:6-7). Huruma yake kwa viumbe wake haina mipaka. Mungu anawaonea huruma wanadamu “si kwa sababu wanamjua, bali ili wamjue; wala si kwa sababu ni wanyofu, bali ili wapate kuwa wanyofu.” Na huruma yake ni mada inayokutwa katika marefu na mapana ya Maandiko Matakatifu ikidhihirishwa kwa namna mbalimbali: kwa njia ya maneno yake, matendo yake, ishara na mifano mbalimbali.
Jicho lake li kwao wamchao
Mtunga zaburi anatufundisha kuwa jicho la Bwana lililo kwao wamchao kuwa ni Mungu mwenye kujua yote, mwangalifu na mwenye ulinzi wa daima (Zab 33:18). Pamoja na mwanadamu kumuasi Mungu mara kwa mara, jicho lake linabaki juu ya kiumbe wake likiendelea kumlinda, kumtunza na kumwalika aache njia mbaya apate kuishi: “Walakini jicho langu likawahurumia nisiwaangamize kabisa wala sikuwakomesha kabisa jangwani” (Ez 20:17).
Hutufariji mfano wa mama kwa mwanae
Manabii Isaya na Hosea wanafafanua huruma ya Mungu kwa lugha ya picha ya mama anayemfariji mwanae. Nabii Isaya anatueleza kuwa ingawa mama anaweza kumsahau mtoto wake anyonyae, Mungu kamwe hatatusahau, na kwa sababu hiyo amemchora kila mmoja wetu katika viganja vyake ili kumtazama na kumtunza daima. “Je, mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyae, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kumsahau, lakini mimi sitakusahau wewe. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu, kuta zako ziko mbele zangu daima” (Isa 49:15-16). Nabii Hosea anatuletea picha ya Mungu wetu mwenye huruma kwa sura ya Mlezi mwenye uvumilivu mkubwa kwa mwana anayekosea tena na tena(Rej. Hosea 11:1-8).
Hutulinda kama Tai alindavyo watoto wake
Ulinzi wa Mungu kwa mwanadamu unaelezwa kwa mfano wa tai anayelinda watoto wake. Hujenga kiota, huwafunika na kuwachukua kwa mbawa zake; “Mfano wa Tai ataharikishaye kiota chake, na kupapatika juu ya makinda yake; alikunjua mbawa zake, akawatwaa, akawachukua juu ya mbawa zake” (Kumb 32:11). Ndivyo Mungu mwenyezi alivyo kwa wana wake. Mwanadamu akitambua huruma ya Mungu isiyo na mipaka hujaribu kutumia lugha yake isiyojitosheleza,ili kueleza jinsi anavyopata malezi, kinga na matunzo bora na ya uhakika.Kanisa linatufundisha kuwa “baada ya dhambi ya Israeli aliyejitenga na Mungu na kuabudu ndama ya dhahabu, Mungu anayasikiliza maombi ya Musa na anakubali kutembea kati ya taifa lisiloaminifu akionyesha hivyo upendo wake.”
Hivyo Mungu wetu daima anadhihirisha upendo wake usio na mipaka kupitia tendo la huruma yake kwa kuwahurumia wanadamu wote. Hata hivyo ingawa “Mungu alituumba bila sisi, lakini hakutaka kutuokoa bila sisi. Kupokea huruma yake hatuna budi kukiri makosa yetu. Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo ndani mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.”

Na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree