BREAKING NEWS

Friday, 12 February 2016

Askofu Gwajima, Sheikh Wa Mkoa Dar Wakwama Kumjulia Hali Mufti

                



Jopo la Madaktari wanaomtibu Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir  wamezuia kwa muda watu kwenda kumtembelea kiongozi huyo wa dini ili apate muda zaidi wa kupumzika.
 
Daktari wake, Profesa Mohamed Janabi jana jioni alisema: “Tumewaomba Mufti aachwe kwa muda ili apumzike. Mimi, Dk Mwanga, Dk Othman na Dk Abel tumeshauri leo (jana) apumzike na kupewa mazoezi zaidi maana watu wa madhehebu yote wamekuwa wengi mno.”

Hatua hiyo ya Dk Janabi ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete alikolazwa Mufti Zubeir, iliwafanya viongozi mbalimbali wa dini akiwamo, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima pamoja na Mbunge wa Kinondoni Mussa Mtulia kushindwa kumwona jana.

Viongozi hao waliowasili katika taasisi hiyo ya Muhimbili saa kumi na moja jioni, walitumia saa nzima kusubiri kama watapata ruhusa ya kumuona Mufti bila mafanikio.

“Nimekuja hapa kumuona Mufti Zubeir kama kiongozi mwenzangu wa kidini, tunamwombea heri apate ahueni,” alisema Askofu Gwajima ambaye baadaye aliamua kuondoka.

Mtulia alisema baada ya kufika hospitalini hapo wamekuta maelekezo kwamba daktari wake ameomba apumzishwe, daktari anataka apone haraka kwani wageni wamekuwa wengi.

“Nilikuja kumwona Sheikh Zubeir baada ya kufika nimeshindwa kumuona baada ya daktari wake kuomba aachwe apumzike, tunaamini tutapata muda wa kumuona baadaye Jumamosi,” alisema Mtulia.

Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), Sheikh Suleiman Lolila alisema jana kuwa hatua hiyo imekuja baada ya kuwapo na watu wengi, ndugu, jamaa na marafiki wanaotaka kumjulia hali na kumfanya akose muda wa kupumzika.

“Hali ya Mufti inaendelea vizuri, tunajua Mufti ni mtu wa watu, lakini tunataka apate muda zaidi wa kupumzika, tunachofanya ni kudhibiti wingi wa watu,”
alisema Sheikh Lolila.

Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree