Daima ikiwa ni jambo jema kushukuru , Baraza la Maaskofu Katoliki la Uganda , Jumanne iliyopita lilikuwa na hafla kwa nia ya kutoa shukurani kwa uongozi wa kisiasa na kidini, kwa kuwezesha ziara ya kihistoria ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Uganda, mwezi Novemba 2015, kuwa ya mafanikio.
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda, Askofu Mkuu John Baptist Odama, wa Jimbo Kuu la Gulu, alitoa shukurani za dhati kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda, wakati wa hafla maalum waliyoiandaa, na kuhudhuriwa na wageni waalikwa zaidi ya 400, akiwemo Waziri Mkuu, Mheshimiwa Ruhakana Rugunda, pamoja na wajumbe wa kamati mbalimbali za maandalizi na viongozi wa ngazi ya juu serikalini na wafadhili.
Askofu Mkuu Odama, katika hotuba yake, pia alifikisha shukurani za Papa Francisko, alizotuma kwa Waganda wote kupitia barua yake kwa Askofu Mkuu Odama, kwa makaribisho mazuri, wema na fadhila walizomwonyesha akiwa Uganda. Na kwamba ziara yake Uganda imemjaza moyo wa matumaini na furaha kutokana na yali aliyojionea, ikiwemo wingi wa watu waliofika kumlaki na kumskiliza, akiitaja hiyo ni ishara nzuri kwamba watu wanahamu ya kukutana na Kristo.
Askofu Mkuu Odama, alikiri kwamba, ziara ya Papa isingekuwa rahisi kufanikiwa hivyo , bila ya ushirikiano wa dhati na bidii ya kila mtu. Na ndiyo maana, Kanisa linatoa shukurani zake za dhati kwa moyo huo wa ushirikiano,na kuongeza, ziara hiyo imewaachia somo muhimu sana kwamba, Kanisa na serikali ni lazima kufanya kazi kwa ushurikiano kwa ajili ya kukuza manufaa ya wote.
Askofu Mkuu alileleza na kutaja kwa namna ya kipekee, shukurani za dhati kwa Ofisi ya Rais, Mawaziri, Polisi, Waamini wa imani dini zingine na uongozi wa Serikali za Mitaa, kwa ajili ya ulinzi mkali na huduma zingine mbalimbali zilizohitajika katika maeneo yote. Na kwamba, mafanikio ya ziara ya Papa imewajengea sifa nzuri Waganda wote, na hivyo ni muhimu wakapania kutunza sifa hiyo kwa kuendeleza ushirikiano waliounyesha, katika lengo la kuwa na umoja, maridhiano na mashauriano, wakati wote.
Na Waziri Mkuu Rugunda akitoa salaam kwa niaba ya serikali alisema, Baba Mtakatifu, amewasha moto mpya wa mshikamano wa kitaifa kwa vitendo, moto wanaopaswa kuudumisha hata wakati wa chaguzi za kisiasa. Alihimiza kufuata mfano wa Papa katika kuwa na moja, kama yeye alivyoonyesha mshikamano wa uekumeni, kwa kiukutana na watu wa madhehebu mengine hata yale yasiyokuwa ya Kikristo . Wajifunzwe kwa jinsi Papa alivyotembelea Madhabahu ya Kianglikan kwa roho safi, ambako alitolea sala na maombi yake. Waziri Mkuu Rugunda, ametaja tukio hilo kuwa ni mfano kwao, wa kuchagua viongozi bila kubaguana kidini.
Post a Comment