BREAKING NEWS

Tuesday, 26 January 2016

Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa: Upendo na utume!



Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa Jimbo kuu la Cebu, Ufilippini linaloongozwa na kauli mbiu “Kristo ndani yenu, tumaini letu la utukufu” limefunguliwa rasmi, tarehe 25 Januari 2016, wakati ambapo Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa. Ni maadhimisho ambayo yanakwenda sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, mwaliko kwa familia ya Mungu kuambata upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma katika maisha na utume wake.

Hili ni tukio la Kikanisa Kimataifa, linalowajumuisha wajumbe na mahujaji kutoka katika nchi 70. Linahudhuriwa na Makardinali 20, Maaskofu 50 kutoka Barani Asia na Maaskofu 100 kutoka Ufilippini. Mahujaji wanahifadhiwa kwenye familia za waamini wapatao 600, ili kuonja upendo wa familia ya Mungu inayowajibika. Itakumbukwa kwamba, hili ni kongamano la pili kuwahi kuadhimishwa nchini Ufilippini. Kwa mara ya kwanza kongamano kama hili liliadhimishwa kunako mwaka 1937 na kwa sasa huko Jimbo kuu la Cebu, Ufilippini.
Kongamano hili la Ekaristi Takatifu Kimataifa nchini Ufilippini lina umuhimu wa pekee kwani Kanisa linaadhimisha Jubilei ya miaka 500 tangu Ukristo ulipoingia nchini Ufilippini kunako mwaka 1521 sanjari na Kumbu kumbu ya Mtakatifu Nino iliyoadhimishwa hivi karibuni nchini Ufilippini. Lengo ni kuimarisha ari na moyo wa kimissionari sanjari na Uinjilishaji mpya unaojikita katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, ili kuwawezesha waamini kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kama anavyosema Kardinali Charles Maung Bo, Mwakilishi wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya. Tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni ni hazina muhimu sana katika mchakato wa Uinjilishaji Barani Asia.
Maadhimisho haya yanapania pamoja na mambo mengine kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho, ili kuzimwilisha katika maisha na utume wa Kanisa, kwani Fumbo la Ekaristi Takatifu lina mwelekeo hata wa maisha ya kijamii yanayojikita katika utunzaji bora wa mazingira; majadiliano ya kidini na kitamaduni ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu pamoja na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, ambao kimsingi ni kiini cha Injili ya Kristo. Hawa ni watu wanaopaswa kuinjilishwa, kushirikishwa na kuhudumiwa kwa upendo na moyo mkuu.
Kongamano la Ekaristi Takatifu Kimataifa ni fursa muhimu sana kwa Kanisa kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na huruma ya Mungu; Injili ya umoja na mshikamano wa familia ya Mungu Barani Asia sanjari na utume wa Kanisa unaojikita katika ushuhuda na Uinjilishaji mpya. Kanisa la kiulimwengu linaungana na Kanisa mahalia Barani Asia, ili kusali, kutafakari, kusikiliza na kushirikiana kwa dhati, ili waamini waweze kujenga nyumba ya Mungu na jirani kati ya watu kwa kujikita katika majadiliano ya maisha, ili kushuhudia Injili ya furaha. Tukio hili limetanguliwa na warsha ya kitaalimungu kimataifa iliyofanyika kwa muda wa siku tatu. Liturujia na utamadunisho; Uinjilishaji katika ulimwengu mamboleo; Ekaristi na majadiliano ya kidini na kitamaduni; Ekaristi na mahusiano na dini mbali mbali ni kati ya mada zinazochambuliwa wakati huu wa maadhimisho ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu kimataifa, litakahitimishwa hapo tarehe 31 Januari 2016.


Share this:

 
Back To Top
Distributed By Rodrick Minja | Designed By Bill De Pierree