Siku moja kabla ya kuanza kwa vikao vya bunge la kumi na moja mjini Dodoma wabunge wametakiwa kuhakikisha wanatumia vema fursa hiyo kuzungumzia masuala muhimu kwa taifa ikiwa ni pamoja na kutafuta suluhu ya mgogoro wa kisiasa mjini Zanzibar.
Wakati macho na masikio ya wengi sasa yakitarajiwa kuelekezwa mjini
Dodoma, wadadisi wa masuala yakisiasa wanasema ni busara kwa wabunge
kutumia bunge kutatua mgogoro wa kisiasa mjini Zanzibar, ikiwa ni pamoja
na kusimamia mijadala yenye lengo la utekelezwaji wa haraka wa malengo
ya serikali ya awamu ya tano.
Wakati serikali ikiendelea na utekelezaji wa hatua zilizotolewa
wakati wa maazimio ya ripoti ya CAG iliyowasilishwa katika bunge la kumi
ambayo ilikuwa ikionyesha uchotwaji wa fedha wa zaidi ya shilingi
bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow, wachambuzi wanasema hilo
pia huenda likapewa uzito wa juu katika bunge la kumi na moja.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na umoja wa makatibu wakuu wa
vyama visivyo na uwakilishi bungeni imewataka wabunge kuwa wamoja katika
kujadili masuala yenye tija kwa taifa na kuachana hoja ambazo tayari
zimekwisha kutolewa maamuzi katika mabunge yaliyopita.
Post a Comment