Ndugu
zangu “lala salama” katika mchezo ni zile dakika za mwisho. Hapo timu
hutupatia picha ya mchezo ulivyokuwa. Kipenga cha mwisho ndicho
kinamtambulisha mshindi. Kadhalika maisha ni lala salama ya kudumu.
Mshindi anajulika kinapopulizwa kipenga cha mwisho wa maisha. Leo tuone
lala salama ya Yesu na wosia aliotuachia wa kuishi vizuri lala salama ya
maisha yetu. Kila mwinjili
anasimulia matukio ya dakika za mwisho za maisha ya Yesu kwa namna yake.
Malengo yao siyo ya kihistoria, bali ni kutufahamisha jinsi Yesu
alivyoishi maisha yake ya upendo na kuyaweka kwa ufupisho dakika za lala
salama. Leo tunampata Luka ndiye anayetusimulia upendo wa Yesu
akitomasa vipengee vya pekee ambavyo Wainjili wengine hawavigusi kabisa.
Mosi, Yesu alisema: “fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.”
Yesu hakumaanisha kurudia tu tendo hilo kiliturujia, bali alitaka pia
kuweka kwa muhtasari maisha yake kwa kujifanya chakula cha maisha ya
uzima wa milele. Sisi turudie kitendo hicho yaani, tuwe mkate kwa ajili
ya wengine. Kipengee cha pili kinahusu ukuu. “Yakatokea mashindano kati yao, kwamba ni nani anayehesabiwa kuwa mkubwa. Akawaambia,“aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule atumikaye. Mimi kati yenu ni kama atumikaye.” Tabia ya kuwania ukuu imetiwa ndani mwetu na Mungu mwenyewe.
Hatuna
budi kujihoji na kuchagua moja au mwono wa kibinadamu wa kuwania ukuu,
au mwono wa Yesu wa kushuka na kutumikia wengine. Sote tungetegemea
katika mazingira haya ya chakula na ya kuwekwa Ekaristi Takatifu,
mazungumzo yangejikita kwenye kuweka mikakati ya kutekeleza sera za Yesu
za kuwa mkate (Ekaristi) kwa ajili ya wengine. Kinyume chake linaibuka
zogo la kuwania ukuu. Hapa tunaalikwa kufanya tafakari ya kina kabla ya
kutoa maamuzi ya Kristo juu ya upendo. Mbinu za kufanikiwa kutoa maamuzi
hayo unayakuta katika kipengee kifuatacho.
Kipengee cha tatu ni kusali. “Ombeni ili msiingie majaribuni.” Yesu mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba. Tatizo
walilokuwa nalo wanafunzi ni kutoa maamuzi ya kutumikia wengine badala
ya kutumikiwa yaani ukubwa. Kwa hiyo dawa ya kushinda kishawishi hicho
ni kusali. Katika lala salama ya maisha yake, hata Yesu mwenyewe alikuwa
katika mapambano ya kutoa maamuzi mazito, kwani shetani alimwonesha
kuwa ameshindwa lakini kumbe katika sala yaani yaani majadiliano na Baba
yake wa mbinguni; katika kuunganika na Baba anapata ushindi. Hapa
tunaoneshwa mbinu za kumshinda shetani kuwa ni sala. Halafu, “Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.”
Katika biblia malaika anaweza kuwa mtu au ufunuo wa moyo au dhamiri
yako inayokuvuvia kutambua maana ya maisha. Hiyo ni kama malaika
anayekupa nguvu ya kushinda udhaifu wa kibinadamu.
Kipengee cha nne ni kutafakari na kukazana kupambana: “Naye
kwa vile alivyokuwa katika dhiki, (mapambano) akazidi sana kuomba; hari
yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka katika nchi. Alipoondoka katika kuomba kwake, akawajia wanafunzi wake, akawakuta wamelala usingizi kwa huzuni. Akamwambia: Ondokeni mkaombe, msije mkaingia majaribuni. Dhiki au huzuni, kwa kigiriki ni agonia na kwa kiingereza ni agony
na maana yake halisi ni mashindano, mapambano, mapigano kama yale ya
wanariadha. Yesu alipambana nayo kutoka mwanzo wa kazi yake kule
jangwani kama dominika ya kwanza ya Kwaresima, yaani mapambano ya kuamua
kumfuata shetani au Baba yake. Unaweza tu kufaulu katika mashindano
hayo kwa sala ya ndani kabisa kama ile ya Yesu. Hiyo ni lala salama ya
kudumu.
Halafu Luka peke yake anasema jasho au hari kama
matone ya damu. Wakati wa mashindano mwanariadha hutoka jasho sana.
Kadhalika Yesu yuko kwenye mashindano makali sana ya ndani ya akili na
moyo hadi anatoka jasho la damu kwani anadhamiria na kufikiria sana.
Hata sisi wakati mwingine tunakuwa katika agony
inapotubidi kufanya maamuzi magumu yanayoumiza na kutupatia machungu
sana. Hasa tunapotakiwa kumsamehe mtu aliyetujeruhi sana hapo tunakuwa
katika mapambano makali sana ndani ya mioyo yetu kati ya kusamehe au
kulipa kisasi. Kwa hiyo kutoka jasho kutokana na kutafakari sana, maana
yake suala la kumshinda mwovu ni suala la kulidhamiria siyo la
kulifanyia mzaha. Hiyo ni lala salama ya kudumu.
Baada ya mapambano hayo makali Yesu anafika na kuwakuta wanafunzi wanaolala usingizi kwa huzuni.
Hapa Yesu hawagombezi wanafunzi wala Petro pale alipowakuta wamelala,
badala yake anawaona hawaelewi uzito wa kipindi cha lala salama kipindi
cha patashika nguo kuchanika hapa ni kusuka au kunyoa!, labda sababu ya
udhaifu wa kibinadamu. Lakini anajua wanampenda licha ya udhaifu wao,
kwa hiyo anabaki kuwaonea huruma na kuwasamehe bure!. Hapa wanaonywa
wachungaji wote kuwa wawasamehe bure na kuwaonea huruma wakosefu na
wadhaifu wote, kwamba wanapenda dini lakini ni wadhaifu Ndiyo maana
katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu,
Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha viongozi wa Kanisa kuonesha ile
sura ya huruma ya Mungu. Mateso ya Kristo yanaonesha ile sura ya huruma
ya Mungu hata kwa wanafunzi wake wanaoelemewa na usingizi wa huzuni.
Kadhalika Wainjili wote wanaeleza kwamba wakati wa mateso ya Yesu mitume
walimkimbia na Yuda alimsaliti lakini Luka peke yake anasema: “Wote waliojuana naye, na wale wanawake walioandamana naye toka Galilaya, wakasimama kwa mbali, wakitazama mambo hayo.” (Lk. 23:49).
Kipengee cha tano ni
kumtendea wema adui. Kipindi cha lala salama, wachezaji wanaweza
kutembeza viatu, kugombana na mchezo ukaisha vibaya. Kwa kikosi cha
kutuliza ghasia, maarufu kama FFU, yaani ”Fanya Fujo Uone” hapani
mkong’oto tu hadi kieleweke! Angalia lala salama ya Yesu alipofika
kushikwa.“Mmoja wao akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume. Yesu Akamgusa sikio akamponya.” Wakati wa kumshika Yesu kulikuwa patashika kubwa. Katika vurugu zile mitume walijipanga kujihami. Wakamwuliza Yesu: “Bwana, tuwapige kwa upanga?” Kwa kweli halikuwa swali, bali walitaka tu uhakika waliposema: “Mzee
inatosha, katika kesi hii kilichobaki ni kuchomoa majambia na kutembeza
visu haiwezekani kufa kikondoo namna hii, lazima tuoneshe kuwa hata
sisi tupo!.” Maana yake uovu na maonezi ni kupambana nayo na kurudisha mashambulio. Kumbe, Yesu anafanya kinyume: “Akamgusa sikio akamponya.” Hapa
tunafundishwa kuwa mkristu anaweza kuwa na wapinzani lakini hatakiwi
kuwa na maadui. Wajibu wa mkristo ni kuwapenda watu wote kwani silaha
haimbadilishi adui. Wakristo wajenge utamaduni wa kusamehe na kusahau
bila kulipiza kisasi, kwani kisasi ni kazi ya Mungu, mwanadamu hana
vigezo sahihi!
Kipengee cha sita: kumhurumia
anayekutukana. Katika lala salama ya mchezo kuna kulaumiana na
kurushiana matusi. Lakini angalia Yesu anapokanwa na kurushiwa matusi “Bwana akageuka akamtazama Petro.”
Wainjili wote wanaonesha jinsi Petro alivyomkana Yesu. Wengine
wanadiriki hata kusema kwamba Petro alitoa hata matusi machafu dhidi ya
Yesu. Hata hivyo “Bwana akageuka akamtazama Petro.” Neno lililotumika la kigiriki ni emblepo,
yaani kutazama kwa undani kabisa kunakogusa dhamiri ya mtu!. Ni sawa na
kumwambia Petro kwamba hata kama umenifanya hivyo, mimi najua
unanipenda. Ndiyo maana Petro anatoka na kulia! Kilio cha mtu mzima si
bure!
Hapa kuna jambo, amekunwa na ”Jicho la
huruma ya Yesu” kama alivyomwangalia yule mwanamke mzinzi, aliyekuwa
amehukumiwa kifo!. Hapa tunafundishwa wakristo jinsi ya kuwaona
wakosefu, na waovu kwa upendo. Kwani wanaweza kuamsha upendo wa mtu
mwovu ukiwaangalia kwa uzuri na wema. Hapa ujumbe ni ”Iweni na huruma
kama Baba yenu”! Hii ndugu zangu ndiyo kauli mbiu inayoongoza
maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu! Injili ya
leo inatupatia muhtasari wa huruma ya Mungu ilivyomwilishwa katika
maisha na utume wa Yesu tangu mwanzo hadi kifo chake Msakabani!
Kipengee cha saba ni kudharauliwa.
Timu inayoshindwa huzomewa na kutupia mayai mabovu!. Hebu angalia Yesu
anavyozomewa. Pilato aliposikia kwamba Yesu ni Mgalilaya akatuma
wampeleke kwa Herode Mgalilaya mwenzake. Huyo alikuwa Herode Antipa,
mtoto wa Herode mkubwa aliyetafuta kumwua Yesu akiwa mchanga, kiasi cha
kutambulika kuwa ”Kizee cha mauaji”. Hebu fuatilia yaliyotokea kwa
Herode Antipa: Kwanza“Herode alipomwona Yesu alifurahi sana.” Herode
alishasikia kuwa Yesu kuwa maarufu kama mganga wa mazingaombwe! Nadhani
wengi mnakikumbuka kile ”Kikombe cha Babu”. Akasubiri kwa hamu sana
kukutana naye ili avione ”laivu” vituko vyake. Pili, “Herode akamwuliza Yesu maneno mengi, yeye asimjibu lolote.” Hapo ikaonekana Herode akawa ”amejisapraisi” mwenyewe, akakata tamaa, na mapato yake sasa: “Herode akamfanya duni, pamoja na askari wake, akamdhihaki, na kumvika mavazi mazuri.” Tafsiri
yake kigiriki ni kwamba alimchamba na kumwona kama ni mwenda wazimu
fulani asiyefaa kwa lolote. Hata wanaomfuata yaonekana
walichanganyikiwa.
Lakini Yesu alikaa kimya hakusema
chochote. Hivyo ndivyo inavyomtokea yule anayetegemea kutendewa miujiza
na Yesu, anakatishwa tamaa kisha anamdharau. Kwa hiyo ieleweke kuwa
ukristo siyo ”supamaketi” au duka la kupata bidhaa, bali ni dini ya
utumishi wa upendo; ni dini ambyo imani yake inamwilishwa katika
matendo, kielelezo cha imani tendaji! Hi isi dini ya miujiza, wale
wanaotaka kuona na kufanyiwa miujiza wana imani haba kama kiatu cha
raba!
Kipengee cha nane ni wa mashabiki wa timu iliyoshindwa. Hapa tunawakuta mashabiki wanyonge kwa ajili ya Yesu mnyonge ni wanawake:“Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea.”
Ingawaje dhambi wametenda wanaume, lakini wanawake ndio wanaoteseka.
Wangesikilizwa zaidi hao, na wanavyoonea huruma pengine vita na maovu ya
duniani yangepungua. Kipengee cha tisa. Majeruhi kwenye lala salama hawakosekani. “Leo hii utakuwa pamoja nami peponi.” Mara
nyingi Yesu alizugukwa na wadhambi na waovu. Mara ya kwanza alipozaliwa
alizungukwa na wachungaji walioeleweka kuwa ni waovu, lakini wakaimbiwa
nyimbo na malaika. Sasa yuko msalabani na wevi lakini mmoja anaahidiwa
paradisi.
Kipengee cha kumi: Yesu akiwa msalabani anasema. “Baba uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo.” Wangelijua
watendalo wasingelifanya. Yesu hatumii lugha mbaya, bali hutoa maneno
ya upendo kwa waovu. Tunaalikwa kuwaangalia vyema wanaokosea badala ya
kuwalaani. Tuwe wanafunzi wanaofanya kama mwalimu wao na kusema: “Baba uwasamehe maana hawajui watendalo.” Kwa hiyo lugha na tendo la mwisho kabisa la Yesu ni Huruma na anatuagiza:“Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi.”
Jamani, iweni na huruma kama Baba wa mbinguni! Kila jema katika
maadhimisho ya kilele cha ufunuo wa huruma ya Mungu katika maisha ya
mwanadamu!
Post a Comment