Kikao
cha siri cha wabunge wa CCM kilichoitishwa juzi usiku kujadili mipango
ya Serikali kudhibiti matumizi, kimefanikiwa kukwamisha uamuzi wa
kuzitaka halmashauri na mashirika ya umma kuingiza mapato yake yote
kwenye mfuko mkuu.
Mpango
huo, ambao pia ulipingwa na wabunge kutoka vyama vya upinzani, ulilenga
kuondoa utaratibu uliopo wa halmashauri, mashirika na taasisi za
Serikali kukusanya mapato yake na kuzitumia na badala yake zilitakiwa
ziingize mapato hayo kwenye mfuko mkuu na baadaye Serikali itoe fedha
kulingana na bajeti inazopelekewa.
Juzi,
katika mjadala wa mwongozo wa Mpango wa Bajeti ya Serikali ya Mwaka
2016/17, wabunge hao walipinga uamuzi huo wakisema utaziua halmashauri
na wakataka mashirika ambayo yanamilikiwa na Serikali ndiyo yapeleke
fedha kwenye mfuko huo.
Kutokana
na mvutano huo, juzi usiku wabunge wa CCM walikutana katika kikao cha
ndani kilichofanyika makao makuu ya chama hicho mjini Dodoma, kujadili
jambo hilo na kushauri libadilishwe ili kuziokoa halmashauri nchini.
Jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene alisema kuwa tayari Serikali imetoa maelezo.
“Tumetoa
maelezo kuwa hatukumaanisha halmashauri wala mifuko ya hifadhi za
jamii. Suala hili litayahusu mashirika ya umma pekee,” alisema Simbachawene.
Habari
kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa wabunge hao walimbana Waziri
wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kwamba uamuzi huo utazifanya
halmashauri kukosa fedha za kufanya miradi yake mbalimbali ikwame.
“Mkutano
ulianza saa mbili usiku na kumalizika saa tano usiku. Tulichokubaliana
na kufanyika kwa marekebisho ili halmashauri ziendelee na utaratibu kama
wa awali, pia kuitaka Serikali kutoihusisha mifuko ya hifadhi za jamii
katika suala hili,” alisema mbunge ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
“Fedha
zitakazokwenda katika mfuko huo ni za mashirika kama Tanesco na
Tanapa.Lengo hapo ni kuweka utaratibu mzuri wa matumizi kwamba shirika
linaingiza fedha zake katika mfuko, likihitaji fedha litapelekewa
kulingana na utaratibu utakaowekwa.”
Chanzo
hicho kilieleza kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii haitaguswa kwa sababu
fedha zake ni za wanachama na hutumika kwa ajili ya kuendesha miradi
mbalimbali.
“Wabunge
pia walihoji kama fedha hizo zitaweza kutoka katika mfuko huo na
kuzifikia halmashauri katika kipindi hiki ambacho fedha nyingi
zinashindwa kufika kwa wakati kutekeleza miradi ya maendeleo,” alisema mbunge mwingine.
Jana,
katika mjadala wa mpango huo hakuna mbunge wa CCM wala wa Ukawa
aliyegusia suala hilo, kitendo kinachotafsiriwa kuwa jambo hilo
limeondolewa kabisa.
Wachangia mjadala
Akichangia
mjadala wa mpango huo, Mbunge wa Lulindi (CCM), Jerome Bwanausi
aliishauri Serikali kuachana na vyanzo vya mapato vilivyozoeleka, badala
yake itafute vyanzo vipya.
Katika
mpango huo, Serikali ilitaja baadhi ya vyanzo vyake vya ndani vya
mapato kuwa ni kodi katika vinywaji mbalimbali, sigara, muda wa matumizi
wa simu za mkononi na kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Katika eneo hilo imeweka uwekezako wa kukusanya Sh4 trilioni. “Watendaji
wa Serikali lazima wajifunze kutoka katika taasisi ambazo zina vyanzo
vingi vya mapato. Mapato yako mengi tu hata katika nyumba za kupanga na
kuziwezesha halmashauri kukusanya mapato zaidi,” alisema.
Mbunge
wa Hanang’(CCM), Dk Mary Nagu alisema uchumi wa viwanda unategemea
kilimo, mifugo na uvuvi na kuitaka Serikali kuhakikisha inatilia mkazo
sekta hizo kwa maelezo kuwa itasaidia kuinua uchumi wa mwananchi mmoja
mmoja.
Mbunge
wa Viti Maalum (Chadema), Anatropia Teonist alionyesha wasiwasi juu ya
utekelezaji wa mipango huo wa Serikali, kutokana na mawaziri wengi
kufanya kazi kwa kutafuta sifa katika vyombo vya habari.
Alimtaja
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kwamba
anahusika katika uporaji wa viwanja vya wananchi.
“Katika
sekta ya ardhi kuna matatizo makubwa. Migogoro ya ardhi inarudisha
nyuma maendeleo ya watu kwa kiasi kikubwa. Pale Dar es Salaam sasa
mnavunja nyumba za watu wa mabondeni. Kutokana na zoezi hilo, zaidi ya
watu 99, 000 watakuwa hawana makazi,” alisema.
Alisema
kasi ya Serikali kuwaletea wananchi maendeleo ni ndogo na kwamba kwa
kipindi cha miaka 15, Serikali imepunguza umasikini kwa asilimia 14 tu.
Post a Comment