Jaji mmoja wa Mahakama ya Juu
nchini Kenya Philip Tunoi amepatikana na hatia ya kukiuka maadili ya
kazi baada ya uchunguzi uliofanywa na kamati iliyoundwa na Tume ya
Huduma za Mahakama.
Jaji Mkuu Willy Mutunga amempendekezea Rais Uhuru Kenyatta aunde jopo maalum kwa mujibu wa Katiba.Jopo hiyo itakuwa na jukumu la kuchunguza kikamilifu madai yaliyotolewa dhidi ya Jaji Tonui.
Kwa mujibu wa katiba, Jaji wa Mahakama ya Juu anaweza tu kuondolewa kazini baada ya kuchunguzwa na jopo.
Jaji huyo anatuhumiwa kupokea hongo ya $2 milioni ili apendelee upande mmoja kwenye kesi ya kupinga kuchaguliwa kwa Gavana wa Nairobi Dkt Evans Kidero.
Dkt Kidero na Jaji Tunoi wote wawili wamekanusha madai hayo.
Iwapo atapatikana na hatia na kuondolewa afisini, atakuwa jaji wa pili wa Mahakama ya Juu kuondoka afisini kwa madai ya kukiuka maadili.
Naibu Jaji Mkuu wa zamani Nancy Baraza alijiuzulu Januari 2012, baada ya jopo kuundwa kuchunguza madai kwamba alimnyanyasa mlinzi wa kike katika jumba moja la biashara jijini Nairobi.
Post a Comment